Habari

Mawakili mashuhuri Katwa Kigeni, Hassan kuhojiwa kuwa majaji

Na JOSEPH WANGUI October 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

TUME ya Huduma ya Mahakama (JSC) imeorodhesha watu 35 kwa nafasi za majaji wa Mahakama ya Rufaa, hatua inayoweza kuwa ya kihistoria baada ya kujumuishwa kwa majaji kutoka mahakama maalum kwa mara ya kwanza.

Kati ya walioteuliwa, 21 ni majaji wa Mahakama Kuu huku 14 wakiwa ni mawakili kutoka sekta ya kibinafsi na taasisi za umma.

Majaji kutoka Mahakama ya Kazi na Ajira walioorodheshwa ni Onesmus Makau, Mathews Nduma Nderi, Linnet Ndolo, Byram Ongaya na Stephen Radido.

Kutoka Mahakama ya Mazingira na Ardhi, walioteuliwa ni pamoja na Yuvinalis Angima, Oscar Angote na Lucy Mbugua.

Mawakili mashuhuri kutoka nje ya mahakama ni Mwenyekiti wa IPOA Ahmed Issack Hassan, wakili Katwa Kigen, na Profesa Migai Akech.

Orodha hii imejiri wiki chache baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali ombi la Seneta wa Busia Okiya Omtatah, ambaye alidai JSC imekuwa ikiwatenga majaji wa mahakama maalum katika uteuzi wa wale wa Mahakama ya Rufaa.

Iwapo uteuzi huu utafanikiwa, idadi ya majaji wa Mahakama ya Rufaa itafika 42, ikiwa bado na upungufu wa majaji 28.Hatua hii inajiri Jaji Mkuu Martha Koome akilenga kupunguza mrundiko wa kesi 5,822 katika mahakama ya rufaa.