Mawaziri wote huru kuenda likizo
Na MWANDISHI WETU
AFISI ya Rais Uhuru Kenyatta imewaruhusu mawaziri wote kuenda likizoni bila kujiamulia kama wangependa kuendelea kuchapa kazi wakati wa shamrashamra za Krismasi.
Ruhusa hiyo ambayo si ya kawaida kwa umma imetokea wakati ambapo duru zinazidi kusema kuna mipango ya kufanya mabadiliko makubwa kwenye baraza la mawaziri.
Mkuu wa Utumishi wa Umma, Bw Joseph Kinyua, aliwasilisha agizo hilo la likizo itakayoanza leo hadi Januari 7, kwenye barua iliyotumwa Desemba 18 kwa mawaziri wote pamoja na Mwanasheria Mkuu Paul Kihara, na makatibu wote wa wizara.
“Mtakapoondoka, mtahitajika kuteua afisa atakayekuwa afisini muda huo wote. Afisa huyo anafaa awe na mamlaka ya kutosha kuendeleza majukumu ya kila siku katika afisi zenu,” ikaeleza sehemu ya barua hiyo.
Hata hivyo, watumishi hao wa umma wameambiwa likizo hiyo si kibali cha kusafiri nje ya nchi kwa kuwa kawaida, wanahitajika waombe ruhusa kabla kufanya hivyo.
Muda mchache kabla tangazo hilo kufichuliwa kwa umma, duru za kuaminika ziliambia Taifa Leo kwamba kuna mawaziri wasiopungua sita ambao huenda watatemwa hivi karibuni.
Tangu aliposhinda uongozi wa taifa kwa awamu ya pili mwaka uliopita, Rais Kenyatta amekuwa akijitahidi kuhakikisha utendakazi wa mawaziri wake utamwezesha kuacha sifa bora atakapokamilisha hatamu yake ya uongozi mnamo 2022.
Masuala makuu ambayo analenga kufanikisha ni vita dhidi ya ufisadi na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo anayoamini itabadilisha hali ya maisha ya Wakenya hasa katika sekta za elimu, afya, makao, miundomsingi na kilimo.
Mara kadhaa, Rais Kenyatta ameshindwa kuficha ghadhabu yake dhidi ya baadhi ya mawaziri anapohutubu hadharani na hii ilidhihirika kwa mara nyingine hivi majuzi alipokuwa Mombasa.
“Ninawaomba mawaziri, tafadhalini, kuwa waziri haimaanishi kukaa afisini. Kuwa waziri si kwamba sasa wewe ni mdosi. Jukumu lako si kuhudhuria mikutano tu. Unahitajika kufanya kazi mahali panapostahili. Kama ni ujenzi wa barabara umekwama, nenda mahali hapo wewe binafsi na uulize kwa nini hili halifanyiki,” akasema.
Endapo rais ataamua kufanya mabadiliko ya baraza lake la mawaziri wakati wa msimu huu wa likizo, inatarajiwa masuala atakayozingatia ni uadilifu, utendakazi na hitaji la kuleta usawa wa kikabila kwenye baraza jipya.
Ikizingatiwa kuwa ana urafiki mpya na Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga na mwenzake wa Wiper Kalonzo Musyoka, itasubiriwa kuonekana iwapo wawili hao watatoa mchango wowote katika uteuzi utakaofanywa.
Kulikuwa na matarajio mengi ya mabadiliko katika baraza la mawaziri Agosti rais aliposafiri Mombasa, lakini akapuuzilia mbali uvumi huo.
Wiki hii, rais hajakuwa nchini kwa muda kwa kuwa alisafiri Vienna, Austria kwa kongamano la ushirikiano wa Afrika na Uropa, huku ikisemekana hana mpango wa kuendeleza desturi ya marais kusherehekea Krismasi na mwaka mpya Mombasa. Bado haijulikani kule ataenda likizoni.