Mbunge amtakia Raila kifo ili Jubilee itawale bila bughudha
Na CHARLES WASONGA
MBUNGE wa Kimilili Didmus Baraza amewashangaza Wakenya kumtakia kifo kiongozi wa ODM Raila Odinga kuhusiana na pendekezo la kuondolewa mamlakani kwa Naibu Rais William Ruto.
Huku akinaswa kwenye kamera za runinga za humu nchini, Bw Barasa alisema, “Watu wengi mashuhuri wamekuwa wakifariki humu nchini. Na mbona huyu Raila Odinga asife ili Jubilee iongoze kwa amani bila usumbufu wa kila mara?”
Mbunge huyo ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto alikuwa akihutubu katika majengo ya bunge, akiandamana na wenzake wenye msimamo sawa, alipokuwa akijibu Seneta wa Siaya James Orengo ambaye Jumatatu alitangaza mipango ya kumwondoa mamlakani Naibu huyo wa rais kupitia hoja katika Bunge la Kitaifa na Seneti.
Akiongea katika eneobunge la Ugenya ambako aliungana na wabunge wengine wa ODM kumpigia debe mgombeaji wa chama hicho Chris Karan, Orengo alisema atawasilisha hoja hiyo kwa sababu “Dkt Ruto amekuwa akiunga mkono ufisadi kinyume cha Katiba na msimamo wa serikali.”
Wabunge hao walioonekana wenye hasira walisema Orengo anatumiwa na Bw Odinga kuendesha mpango huo unaoelenga kusambaratisha Jubilee.
“Raila anataka kumwondoa Ruto ili atwae kiti hicho cha Naibu Rais. Hii ndio maana anatumia mtu wake wa mkono James Orengo kuwasilisha hoja hiyo,” akasema Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro.
“Kama Orengo ni mwanaume hebu awasilishe hoja hiyo aone vile itaangushwa. Ningependa kumwambia Raila na wenzake katika ODM kwamba Ruto ana uungwaji mkono mkubwa zaidi katika mabunge yote mawili,” akaongeza Bw Nyoro.
Bw Barasa alidai kuwa hoja hiyo hailengi tu Bw Odinga bali inalenga kumwangusha Rais Uhuru Kenyatta na serikali yake yote.
Bw Barasa alisema Bw Odinga ni tapeli ambaye anatumia vita dhidi ya ufisadi kwa lengo la kuzima ndoto ya Dkt Ruto kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2022.