Habari

Mbwembwe za Mwaka Mpya 2019

January 1st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na WAANDISHI WETU

MAMILIONI wa Wakenya kote nchini usiku wa kuamkia Jumanne waliungana na wenzao ulimwenguni kuukaribisha mwaka mpya wa 2019 kwa mbwembwe na furaha huku wakiwa na matumaini ya kupata ufanisi maishani.

Wengi walijumuika makanisani na misikitini kushiriki sala za kushukuru Mungu kwa kuwawezesha kuuaga mwaka wa 2018 na kuombea mafanikio katika mwaka huu.

Vilabu vya burudani navyo vilifurika wananchi waliojiburudisha kwa muziki wa bendi na shoo za wasanii mbalimbali. Fataki zilitanda angani kote mshale wa saa ulipoashiria saa sita kamili na kufuatiwa na mbwembwe, hoi hoi na vifijo.

Zilikuwa sherehe za kipekee katika kilabu cha Eldoret Sports Club pale wakazi walipocheza kwa shangwe na nderemo za kuukaribisha mwaka 2019. Picha/Jared Nyataya

Jijini Nairobi, msanii wa nyimbo za bongo Naseeb Abdul Juma, almaarufu Diamond Platinumz, alitumbuiza katika tamasha ya Wasafi Festival katika Uhuru Gardens. Mtanzania huyo ni miongoni mwa wasanii wa kigeni na wa humu nchini waliowaongoa wananchi katika tamasha hiyo. Maafisa wa usalama walishika doria kote jijini na viungani ili kukabiliana na wahalifu.

Mjini Mombasa, nyota mwingine wa bongo, Ali Kiba na bendi ya Sauti Sol waliwaburudisha mashabiki wao katika ukumbi wa Mombasa Sports club katika tamasha ya NRG Wave Showdown. Wanamuziki wengine waliowaongoa wapenda muziki ni Fena Gitu an Gilad huku Dj Kace akiporomosha ngoma motomoto.

Usalama uliimarishwa katika hoteli kadhaa za Mombasa ambazo zilijaa watalii kutoka humu nchini na mataifa ya kigeni. Wateja walikaguliwa kabla kuruhusiwa kuingia katika hoteli za Travellers Beach, Sarova Whitesand na nyinginezo katika maeneo ya Diani, Watamu na Malindi.

Wakristo wakiadhimisha ibada ya Mwaka Mpya katika kanisa la Talents Revival Church eneo la Elburgon, Nakuru. Picha/John Njoroge

Watu wa matabaka mbalimbali, waume kwa wake, walifurika katika ufuo wa Jomo Kenyatta kwa sherehe ya ufyatuaji wa fataki. Katika kaunti ya Makueni, wakazi walilaki mwaka mpya kwa densi, nyimbo na sala katika uwanja wa Unoa mjini Wote.

Tamasha hiyo iliwaleta pamoja wasanii mbalimbali wa injili, kwaya na wahubiri kutoka makanisa na misikiti mbalimbali.Baadhi ya viongozi wa kisiasa waliohudhuria tamasha hiyo kwa jina Sifa Blast; ni Gavana Kivutha Kibwana, Spika wa Bunge la Kaunti ya Makueni Douglas Mbilu na wabunge Erustus Kivasu (Mbooni), Joshua Kimilu (Kaiti) na Daniel Maanzo (Makueni).

Mwanamuziki maarufu wa nyimbo za Bongo, Mtanzania Ali Kiba atumbuiza wafuasi wake katika uwanja wa Mombasa Sports Club wakati wa shamrashamra za kuukaribisha Mwaka Mpya wa 2019 mkesha wa kuamkia Mwaka Mpya. Picha/Kevin Odit

Wasanii wa nyimbo za injili walioongozwa na Bi Mercy Masika ambaye ni mzaliwa wa kaunti ya Makueni. Pia alikuwepo msanii wa umri mdogo wa miaka 10, Shukrani Waeni. Gavana Kibwana, Askofu Mkuu Timothy Ndambuki, wa kanisa la ABC na mwenzake wa kanisa la Christian Impact Mission, Titus Masika, walihimiza wananchi kutia bidii katika mwaka wa 2019 ili kuzidisha ufanisi ambao kaunti hiyo iliandikisha katika nyanja za maendeleo mwaka jana.

“Makueni ina jina zuri. Tunasifiwa kote nchini. Tushukuru Maulana ili atupe uwezo na nguvu ya kupata ufanisi mwingine katika mwaka huu wa 2019,” akasema Profesa Kibwana.

Mwanamuziki maarufu wa Tanzania, Naseeb Abdul Juma almaarufu Diamond Platnumz atumbuiza mashabiki wake katika bustani ya Uhuru Gardens, Nairobi katika tamasha ya Wasafi Festival mnamo Jumatatu, usiku wa kuamkia sikukuu ya Mwaka Mpya jana. Picha/Dennis Onsongo

Na katika kaunti ya Bungoma, viongozi wa kidini walipongeza salamu za heri kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa upinzani Raila Odinga, wakisema hatua hiyo iliwezesha amani kudumu nchini mwaka wa 2018. Wakiongozwa na Askofu wa Kanisa la Kianglikana Dayosisi ya Bungoma George Mechuma, viongozi hao waliwataka viongozi wa kisiasa kote nchini kuiga mfano wa vinara hao wawili.

“Tumeweza kukamilisha mwaka wa 2018 kwa amani baada ya Rais Kenyatta na Odinga kusalimia na kuridhiana mnamo Machi 9,” akasema Askofu Mechumo.

Akaendelea: “Tukiingia mwaka wa 2019, kama kanisa, tunapaswa wakuwauliza viongozi wetu wa kisiasa kuiga mfano wa wawili hao kwa kupunguza joto la kisiasa.”

– Ripoti za Charles Wasonga, Eunice Murathe, Pius Maundu na Denis Lubanga