Mfadhili wa nishati ya upepo Lamu atisha kujiondoa
NA KALUME KAZUNGU
MFADHILI mkuu wa mradi wa nishati ya upepo, Kaunti ya Lamu ametisha kujiondoa katika kutekeleza mradi huo kutokana na vikwazo vinavyoelekezewa mradi huo hasa kutoka kwa kampuni ya umeme, Kenya Power.
Mradi huo wa gharama ya Sh 21 bilioni uko chini ya ufadhili wa kampuni ya Ubelgiji ya Elicio kwa ushirikiano na Kenwind Holdings Limited ya humu nchini.
Mradi huo unatarajiwa kuzalisha megawati 90 za umeme punde utakapokamilika.
Katika mahojiano ya kipekee na Taifa Leo Dijitali Jumanne, Mkurugenzi Mkuu wa mradi huo, Susan Nandwa alisema tayari bodi ya usimamizi na ufadhili wa mradi huo yenye makao makuu nchini Ubelgiji imetisha kujiondoa kufuatia utata unaoendelea kughubika mradi huo, ikiwemo kutolewa kwa hati ya kukubali kuendelezwa kwa mradi huo (PPA) inayostahili kutiwa kukubaliwa na kutiwa saini na KPLC.
Kulingana na Bi Nandwa, KPLC haijaweka saini hati hiyo licha ya kupewa amri na Tume ya Kawi nchini (ERC) kufanya hivyo.
Bi Nandwa anasema hatua hiyo inachangia kuendelea kucheleweshwa kuanza kwa mradi huo.
“Tunashangaa kwa nini KPLC haitaki kukubali kutia saini hati ya PPA licha ya kwamba ERC ilitoa ruhusa wafanye hivyo. Mradi ulistahili kuanza tangu 2016 lakini hadi sasa hatujaweza kufanya hivyo kutokana na pingamizi zilizoko. Watupe P.P.A kwani tayari bodi ya kufadhili mradi tayari imetoa onyo kwamba huenda ikajiondoa iwapo tutaendelea kusumbuliwa,” akasema Bi Nandwa.
Wakati huo huo, wakulima wa eneo kunakolengwa kuanzishwa mradi huo huko Baharini wanaitaka serikali na mwekezaji kueleza wazi iwapo mradi utatekelezwa eneo lao.
Wakulima hao walisema wamechoka kusubiri fidia ya ardhi zao zilizotwaliwa kufanikisha ujenzi wa mradi huo.
Wakiongozwa na Bw Joseph Mwangi, wakulima hao waliitaka serikali na mwekezaji kuharakisha fidia hiyo au wawarudishie ardhi zao ili waziendeleze.
“Tumechoka kusubiri fidia. Watueleze iwapo mradi utatekelezwa au la. Tunalotaka ni fidia zetu au ardhi zetu iwapo mradi umeshindikana,” akasema Bw Mwangi.
Naye Bi Lucy Kaguthe, alisema benki zimedinda kuwapa mikopo wakitumia hatimiliki za mashamba yao kutokana na kwamba tayari ardhi ya Baharini inaashiria kwamba ni ya kiwanda cha nishati ya upepo.
Jumla ya ekari 3,206 eneo la Baharini zimetwaliwa kufanikisha ujenzi wa kiwanda hicho.