Mgawanyiko ODM unatatiza uongozi wangu – Dkt Oburu
KIONGOZI wa ODM, Dkt Oburu Oginga, amewataka viongozi wazime mgawanyiko wakati ambapo tofauti zinazidi kuhusu chama kumuunga au kutomuunga Rais William Ruto kwenye uchaguzi mkuu wa 2027.
Akiongea wakati wa ibada ya Krismasi katika St Peter ACK Bondo, Kaunti ya Siaya, Dkt Oginga alisema kuongoza ODM ni jukumu gumu na atafanikiwa tu iwapo atapata uungwaji mkono wa wabunge na kuzimwa kwa maasi ya ndani.
“Hili jukumu ni zito na nitafanikiwa tu mkiwa nyuma yangu. Nitawatumikia tu mkiniunga mkono hata kama sitoshei ndani ya viatu vya Raila Odinga,” akasema.
Seneta huyo wa Siaya alisema hana nia ya kuongoza kwa udikteta akisema ODM itafanikiwa kusalia na umaarufu kupitia tu maoni kinzani kuvumiliwa na mashauriano.
“Sitaki hali ambapo Dkt Oburu akisema tuende kushoto au kulia inakua hivyo. Lazima tushauriane, tuchukue msimamo mmoja na tuzungumze kwa sauti moja,” akasema.
Seneta huyo wa Siaya alipuuza madai kuwa ODM inaendelea kupoteza umaarufu wake akisema wanamakinikia kupigania maslahi ya Wakenya.
“Hiki chama hakitagawanyika wala kusambaratika. Kinaendelea mbele kupigania haki za Wakenya na hakuna kurudi nyuma,” akasema.
Licha ya kutounga mkono Rais Ruto kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, Dkt Oginga alisema watasalia ndani ya Serikali Jumuishi hadi 2027.
“Tuko serikalini huku tukijiimarisha. Hii serikali tuliingia kupitia dirishani kwa sababu hatukuichagua na tutashirikiana nayo hadi 2027,” akasema huku akishikilia hoja 10 zilizo msingi za muungano wao na UDA lazima zitekelezwe.
Dkt Oburu ambaye alihudumu kama Mbunge wa Bondo kutoka 1994 hadi 2013, alisema kuwa ODM ipo serikalini kuhakikisha maeneo yao yananufaika na miradi ya serikali baada ya kubaguliwa na tawala za nyuma.
“Kitambo tufike 2027, maeneo yetu yatakuwa yameendelea na unaona jinsi ambavyo Rais Ruto anavyojizatiti,” akasema.
Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa ibada kuandaliwa katika kanisa hilo baada ya mauti ya Kiongozi wa upinzani Raila Odinga mnamo Oktoba 15.
Raila, Dkt Oginga na familia ya Jaramogi wamekuwa wakihudhuria ibada ya Krismasi kanisani humo kila mwaka.
Dkt Oginga aliandamana na Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi na Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ya Kisumu Ruth Odinga, dadake Raila pamoja na wanasiasa wengi kutoka Nyanza.
“Kile ambacho Rais Ruto anatupa ni kilicho chetu wala hatujakuwa cha mwingine. Miradi yote tunayopewa tunastahili kuwa nayo,” akasema.
Wiki jana, Dkt Oginga alisema kuwa ifikapo Juni 2026, ODM itakuwa imefanya uamuzi wa kumuunga au kutomuunga mkono Rais mnamo 2027.
Kauli yake ilipingwa na Gavana wa Siaya, James Orengo na Katibu wa ODM, Edwin Sifuna ambao walisema kazi ya kuamua mkondo ambao chama kitachukua kuhusu 2027 si suala la kuamuliwa na mtu mmoja.
Hata hivyo, Bw Wandayi amesisitiza kuwa katiba ya ODM inampa kiongozi wa chama mamlaka ya kuamua mwelekeo na uamuzi huo unastahili kuidhinishwa na ngazi za chama.
“Kiongozi wa chama ana jukumu la kuongoza chama na wanachama kwenye majadiliano ya miungano. Baada ya kufanya uamuzi huo, unawasilishwa kwa Baraza Kuu la Chama na kuidhinishwa,” akasema Bw Wandayi.
Waziri huyo alimtaka Dkt Oginga atoe mwekelekeo huo kufikia Machi mwaka ujao badala ya Juni kuepusha wafuasi wa ODM kuchanganyikiwa.