Mijadala ya ufisadi yafunika njaa inayotafuna maelfu ya wananchi
WAANDISHI WETU
HUKU wanasiasa wakiendelea kurushiana cheche katika mikutano ya mazishi na harambee kuhusu wizi wa mabilioni, Wakenya zaidi ya milioni moja walio hatarini kufa njaa wamesahaulika.
Tayari jumla ya watu saba wameripotiwa kufariki na idadi hiyo huenda ikaongezeka ikiwa hatua hazitachukuliwa kuwapa misaada ya chakula.
Watu saba wameripotiwa kufariki kwa kukosa lishe katika kaunti ndogo ya Tiaty, Kaunti ya Baringo huku maelfu ya wananchi wakiendelea kuathirika katika kaunti 23 zinazokumbwa na kiangazi kote nchini.
Uchunguzi wa Taifa Jumapili ulionyesha kuwa, mito imekauka huku wafugaji wakilazimika kuhamia kaunti jirani kusaka maji na lishe hali inayoibua hofu ya kutokea kwa mapigano ya kijamii.
Katika kaunti ya Baringo, wakazi hawana tabasamu kama viongozi wao, nyuso zao zimedhoofika kwa njaa, huku watoto, wazee na akina mama waja wazito wakiathirika zaidi.
Maeneo yaliyoathiriwa zaidi ni wadi za Silale na Kositei ambapo watu wanne walifariki na kufuatiwa na wengine watatu baada ya kuathiriwa na makali ya njaa.
Chifu wa kata ndogo ya Kositei, Jack Ronei alisema hali ni mbaya zaidi na kuitaka serikali kusambaza chakula cha msaada ili kuzuia maafa zaidi.
Alisema waliofariki wanatoka vijiji vya Kamusuk, Kositei na Seretion ambako watu wanne waliangamia. Maeneo mengine yaliyoathirika zaidi ni Chematony, Tobereruo, Panyirit, Kopoluo, Kadeli, Korio na Katikit.
Chifu Ronei aliwatambua waliofariki kama Chemkea Limo, Stephen Lokdap, Akileng’ Limere na Chepokughe Akuruona.
Waathiriwa sasa wameamua kula matunda ya mwituni kwa jina ‘Sorich’ ambayo huchemshwa kwa saa nyingi ili kuondoa sumu.
Bw Domoo Nakule ambaye ni mkazi wa eneo hilo alisema wanawake hulazimika kusafiri mwendo mrefu kusaka matunda hayo ambayo huchemshwa mchana kutwa kuondoa sumu kabla ya kula.
“Matunda hayo ya mwituni huchemshwa kando ya mto kwa sababu yanahitaji maji mengi kuondoa sumu hiyo. Hata hivyo, watoto na wakongwe bado hutapika na kuhara baada ya kula matunda hayo lakini hawana jingine kwa sababu hakuna chakula kingine,” akasema Bw Nakule.
Katika kijiji cha Kamusuk, tulimpata Mzee Lochoria Karani mwenye umri wa miaka 70 akilala chini ya mti akitafakari cha kufanya. Jana, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO) yalitaka serikali, na wadau wengine, kuweka mikakati ya kudumu itakayohakikisha maafa hayatokei nchini kutokana njaa na majanga mengine.
“Tunaomba serikali kuweka mipango ya kuhakikisha uzalishaji chakula unaimarishwa na hivyo kuzuia maafa kama yaliyoripotiwa Baringo,” alisema Mwenyekiti wa Baraza la Mashirika hayo Stephen Cheboi kwenye taarifa.
Na katika Kaunti ya Turkana, vijiji vilivyoathirika zaidi na baa la njaa ni pamoja na Nakurio na Kapua katika eneo bunge laTurkana ya Kati, Kapedo na Katilia katika eneo bunge la Turkana Mashariki na Kalapata katika eneo bunge la Turkana Kusini. Maeneo mengine yaliyoathiika ni;Loteteleit katika eneo bunge la Loima, Kataboi na Lokitaung katika eneo bunge la Turkana Kaskazini.
Gavana wa kaunti hiyo Josephat Nanok alisema ukosefu wa mvua kwa zaidi ya miezi tisa na uvamizi wa nzige zimechangia kiangazi katika maeneo kadhaa.
“Kiangazi hiki kimesababisha zaidi ya wafugaji 30,000 kutoka hapa kwetu kwenda Uganda kusaka maji na lishe,” Bw Nanok alisema.
Katika kaunti za Makueni na Kitui, maelfu ya wananchi wanakabiliwa na baa la njaa baada ya mvua fupi ya kati ya Novemba na Desemba mwaka 2018 kufeli na hivyo kuathiri mimea ya chakula.
Maeneo yalioathirika zaidi ni kaunti ndogo za Kitui Mashariki, Mwingi, Kibwezi na Makueni pamoja na maeneo ya nyanda za chini ya kaunti ndogo ya Mbooni.
“Nyakati nyingi huwa tunashinda bila kula chochote. Hii ni kwa sababu mahindi yetu yaliharibiwa na kiangazi mwaka jana na sisi hutegemea vibarua kwa sababu hamna mmoja wetu aliye na ajira ya mapato mazuri,” akasema Bi Mutinda Ndeke, mjane anayeishi katika kijiji cha Mweini.
Wakati huo huo, mito inaelekea kukauka huku uhaba mkubwa wa maji ukishuhudiwa katika kaunti ya Narok na kuhatarisha maisha ya binadamu, mifugo na wanyama pori katika mbuga maarufu ya Maasai Mara.
FLORA KOECH, SAMMY LUTTA, PIUS MAUNDU, GEORGE SAYAGIE, BONIFACE MWANIKI na CHARLES WASONGA