Mikutano ya uhamasisho BBI iwe na utaratibu mzuri – Karua
Na PETER CHANGTOEK
KIONGOZI wa chama cha Narc Kenya, Bi Martha Karua, amewalaumu viongozi ambao huiandaa mikutano ya hamasisho la mpango wa maridhiano (BBI), kwa kile alichokitaja kuwa kutowaalika wale wanaoaminika kuwa na mtazamo tofauti.
Akiwahutubia wanahabari jijini Nairobi leo Ijumaa, kiongozi huyo amesema hajawahi kualikwa hata siku moja kwa ajili ya mchakato huo.
“Sijawahi kualikwa pahala popote katika eneo la Kati,” amesema Karua.
Ameongeza kuwa kuna woga miongoni mwa waandalizi kuhusu maoni yanayokinzana na baadhi ya viongozi walio mstari wa mbele katika mchakato huo.
“Wanaoiaandaa huwaalika viongozi wanaoegemea upande wao. Mimi mwenyewe siegemei upande wao katika eneo la Kirinyaga na sijawahi kualikwa mahali popote katika eneo la Kati kwa sababu wanajua mtazamo wangu,” amesema Bi Karua.
Ameongeza kusema kuwa ni watu wachache mno ambao wameisoma ripoti hiyo ya BBI.
“Baadhi yetu tumesoma ripoti hiyo kwa simu zetu za Smartphone. Je, kila mtu ana simu za Smartphone au vifurushi vya dat ili kusoma ripoti hiyo?” ameuliza.
Aidha, kiongozi huyo ameshangaa kwa nini Kenya inalegeza msimamo wake kuhusu raia wa China na ndege za kutoka nchini humo zinazoingia nchini wakati kuna virusi hatari vya Corona.