HabariSiasa

Miradi iliyokwama yageuka silaha dhidi ya Ruto

March 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 5

Na WAANDISHI WETU

KUKWAMA au kujivuta kwa utekelezaji wa miradi iliyozinduliwa na Naibu Rais William Ruto mwaka 2018 katika kaunti nyingi, kumegeuka silaha ya maadui wake wa kisiasa.

Miradi hiyo, ambayo mingi ni ya ujenzi wa barabara, haijaanza ama utekelezaji wake unaendeshwa polepoke, kiasi cha kuzua malalamishi kutoka kwa wananchi.

Hali hii imewapatia wapinzani wake fursa ya kudai kuwa “miradi hiyo ni hewa” na DSkt Ruto alikuwa na nia ya kujijenga kisiasa.

Lakini wachanganuzi wanasema huenda Dkt Ruto alitegwa na baadhi ya maafisa wa serikali kuzindua hiyo, kwa hakikisho kuwa ilikuwa kwenye mipango ya serikali, wakifahamu kuwa hakukuwa na pesa za kuifadhili, na hivyo ingekwama na kumharibia sifa “kwa kuhadaa wananchi”.

Wengine nao wanasema Naibu Rais alianzisha miradi hiyo akiwa na hakikisho la ufadhili, lakini ikavurugwa na hatua ya Wizara ya Fedha kusimamisha utekelezaji wa miradi mingi nchini, kutokana na madeni ya kigeni na kupungua kwa pesa za kufadhili bajeti.

Katika uchunguzi wa Taifa Leo katika kaunti za Nyeri, Kirinyaga, Kiambu, Kisii, Nyamira, Migori na Kakamega, ilijitokeza kuwa wananchi wameanza kukosa matumaini ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Katika Kaunti ya Nyeri, baadhi ya miradi ya ujenzi wa barabara iliyoanzishwa na Dkt Ruto mwaka jana imeanza, lakini inaendelea kwa mwendo wa kinyonga.

Katika eneo bunge la Kieni, Dkt Ruto alizindua ujenzi wa barabara tatu ya thamani ya Sh4.4 bilioni mwaka jana.

Wakazi wanasema wanakandarasi wanajivuta licha ya ahadi kwamba wangekamilisha kazi hiyo katika kipindi cha mwaka mmoja.

“Wanakandarasi hao hawajaonyesha kujitolea katika utekelezaji wa miradi hii. Nyakati zingine huwa wanatoweka kwa muda wa miezi miwili hali inayotufanya kushuku ikiwa ujenzi wa barabara hizo utawahi kukamilishwa,” akasema mkazi kwa jina Samuel Kariuki.

Kwa mfano, mwanakandarasi anayejenga barabara ya Kanyagia – Endarasha ya umbali wa kilomita 13 anaendesha kazi kwa mwendo wa kinyonga. Wafanyakazi wa mikono huonekana wakichimba mitaro kando mwa barabara huku matingatinga yakiwa yameegeshwa katika kituo cha biashara cha Endarasha.

Hata hivyo, mbunge wa eneo hilo Kanini Kega anasema mwanakandarasi amepewa miezi tisa kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo ya Kanyagia – Endarasha na akapinga madai kuwa utekelezaji wa kazi hiyo umecheleweshwa.

Bw Kega anawashutumu wanaodai kuwa Dkt Ruto alizindua miradi ‘hewa’ akisema wakazi wa eneo bunge lake wameridhika.

Mwenzake wa Mathira, Rigathi Gachagua pia anatetea miradi hiyo, akieleza kuwa hivi karibuni barabara mbili zitajengwa katika eneo bunge hilo kwa gharama ya Sh3 bilioni.

“Barabara ya Marua – Kiamariga ya umbali wa kilomita 43 inayoelekea katika Ikulu ndogo ya Sagana, ni miongoni mwa barabara ambazo zitawekwa lami mwaka huu. Mamlaka ya Barabara za Mashambani (KERRA) ilitangaza kandarasi yake mwezi uliopita,” anasema Bw Rigathi.

Mnamo Januari 12, 2018, akihudhuria mazishi katika Kaunti ya Kiambu, Dkt Ruto alitangaza kuwa utawala wa Jubilee utatenga Sh800 milioni kwa ajili ya ukarabati wa barabara ya Marige – Gathiruini. Lakini kufikia sasa hakuna chochote ambacho kimefanyika katika barabara hiyo ya umbali wa kilomita 23.

Miradi mingine ambayo imezinduliwa na Dkt Ruto katika Kaunti ya Kiambu ni ujenzi wa barabara ya umbali wa kilomita 47 ya Uplands – Githunguri – Ruiru, ambayo inakadiriwa kugharimu Sh4.6 bilioni. Kazi ilianza katika barabara hii lakini ikasimama mapema mwaka huu.

Pia kuna barabara ya Githunguri – Kagwe – Kimende ya umbali wa kilomita 26 na ambayo inatarajiwa kugharimu Sh2.4 bilioni. Wakazi wanasema kuwa matingatinga yaliyotumika wakati wa uzinduzi wake yaliondolewa baada ya muda mfupi.

“Inaonekana tulikuwa tukichezewa kwa sababu tangu Septemba mwaka jana hakuna hata futi moja ya barabara imechimbwa, na matinga yaliondolewa siku chake baadaye,” Bw James Kioge, mkazi wa eneo la Kagwe anasema.

Dkt Ruto pia alizindua ujenzi wa barabara Wangige – Nyathuna – Ngecha inayopita katika ya maeneo bunge ya Kabete na Limuru, lakini ujenzi haujaanza.

Katika kaunti ya Kiranyaga, wakazi pia wamelalamikia kucheleweshwa kwa miradi ya barabara iliyozinduliwa mwaka jana na Naibu Rais. Wanasema barabara za Njegas – Kianjege na Ngaru – Gikoigo bado ziko katika hali mbaya.

Wakazi pia wanalalamika kuwa ujenzi wa barabara ya Kutus – Kiamutugu katika eneo bunge la Gichugu kwa gharama ya Sh1.2 bilioni, iliyokaguliwa na Naibu Rais mwaka jana umekwama.

Mwanakandarasi mmoja aliyepewa kazi hiyo miaka miwili iliyopita alisitisha kazi baada ya kuweka lami umbali wa kilomita tano pekee. Mwezi jana wakazi wa eneo hilo walitisha kufanya maandamano kulalamikia kukwama kwa mradi huo.

Katika Kaunti ya Migori, wananchi wanasema mingi ya miradi ambayo Dkt Ruto alisema serikali ya kitaifa itaanzisha katika kaunti hiyo haijaanzishwa, miezi kadha baada ya kuzinduliwa.

Mwaka jana Dkt Ruto alizuru Migori mara tano, akitoa ahadi mbalimbali za maendeleo. Alifufua upya ujenzi wa barabara ya Kehencha – Migori – Masara, ambayo ilikwama kabla ya kufika katika eneo la Muhuru Bay katika kaunti ndogo ya Nyatike. Kufikia sasa ujenzi huo haujaanza licha ya Dkt Ruto kuahidi kuwa mwanakandarasi angeanza kazi Januari mwaka huu.

Wakati wa ziara hiyo, Naibu Rais pia aliahidi kuwa serikali kuu itaanzisha ujenzi wa vyuo vya kiufundi katika maeneo bunge ya Suna Magharibi na Nyatike. Wakati huo aliwataka wabunge Peter Masara (Suna Mashariki) na Tom Odege (Nyatike) kufika afisini mwake kuchukua pesa za kuanzisha miradi hiyo.

“Aliahidi kuanzisha chuo cha kiufundi katika eneo la Masara, lakini kufikia sasa hajatimiza ahadi hiyo. Tumejaribu kumfikia lakini bado tunasubiri,” Bw Masara akasema.

Katika eneo la Kuria, wakazi wamelalamikia kutotimizwa kwa ahadi za maendeleo zilizotolewa kuanzia 2017.

Mnamo Novemba, mwaka jana, Naibu Rais alifungua rasmi chuo cha kiufundi cha Kedenge, ambacho alisema kitaanza kuwasajili wanafunzi Januari mwaka huu. Lakini miezi miwili baada ya kufunguliwa, chuo hicho kingali hakina wanafunzi na hamna shughuli zozote zinazoendelea humo.

Akiwahutubia wananchi wakati huo, Dkt Ruto aliahidi kuwa serikali kuu ingetoa ruzuku ya Sh100 milioni kuimarisha miundo msingi katika mji wa Kehancha. Pia aliahidi kuwa Wizara ya Afya itapeleka mtambo wa CT scan katika Hospitali ya Rufaa ya Migori. Lakini mpaka sasa ahadi hizo hazijatimizwa.

Hata hivyo, Mbunge wa Kuria Mashariki, Marwa Kiyatama, amemtetea Naibu Rais akishikilia kuwa miradi yote aliyoahidi itatekelezwa: “Dkt Ruto ana nia njema kwa watu wa Migori. Sina tashwishi kwamba atatimiza ahadi zake,” akasema Bw Kitayama.

Akaongeza: “Miradi yote aliyoanzisha itatekelezwa. Watu wetu wanafaa kuwa na subira. Kwa mfano tayari ujenzi wa barabara ya Isebania – Kehancha – Kegonga utaanza hivi karibuni.

Vile vile, anasema kuwa tayari mwanakandarasi kutoka China ameanza ujenzi wa barabara ya Kehancha – Kegonga – Ntimaru inayopita kati ya maeneo bunge ya Kuria Magharibi na Mashariki.

Lalama pia zimechipuza katika kaunti jirani za Kisii na Nyamira, ambapo wakazi wanadai miradi iliyozinduliwa na Naibu Rais tangu 2016 inatekelezwa kwa mwendo wa kinyonga ama imekwama.

Mfano ni ujenzi wa bewa la Ibeno la Chuo cha Mafunzo ya Matibabu (KMTC) lililoko eneo la Nyaribari, uliozinduliwa mnamo 2016, na bewa la chuo hicho hicho la Bomachoge Chache, lililozunduliwa Oktoba mwaka jana.

Mbunge wa Bomachoge Chache, Alfa Miruka, anasema japo kazi ya ujenzi wa bewa la KMTC imekuwa ikiendeshwa polepole, itakamilika kabla ya Juni 30, mwaka huu: “Huu ni mradi wa mwaka wa kifedha wa 2018/2019 na tuna furaha kwamba umeanza kwa sababu ulitengewa pesa. Pesa za kuukamilisha zitatolewa na serikali ya kitaifa,” akasema.

Katika eneo bunge la Kitutu Masaba, Kaunti ya Nyamira, ujenzi wa barabara ya Kiendege – Emberge- Gachuba – Keumbu haujaaza licha ya kuzinduliwa na Naibu Rais mwaka jana.

Hata hivyo, Mbunge wa eneo hilo Shadrack Mose ametetea kucheleweshwa kwa utekelezaji wa miradi iliyozinduliwa na Dkt Ruto, akisema japo haijaanzishwa kwa wakati, itakamilishwa kabla mwaka huu kuisha.

“Katika muda wa mwezi mmoja ujao, kazi itaanza katika mradi huu. Nimekuwa nikishauriana na wahandisi kila mara. Miradi ya serikali haiwezi kuzinduliwa bila mpango,” akasema Mbunge huyo.

Katika eneo bunge la Bobasi, Wizara ya Michezo haijanzisha Chuo cha Michezo katika eneo la Nyachogochogo kama alivyoahidi Naibu Rais alipozuru eneo hilo Juni mwaka jana.

Hata hivyo, mbunge wa Mugirango Kusini, Sylvanus Osoro anasema ni wajibu wa viongozi waliochaguliwa kufuatilia na kuhakikisha kuwa miradi ya serikali imetekelezwa ilivyopangwa.

“Tunapaswa kukoma kuendelea dhana kwamba miradi ya serikali imekwama au inatekelezwa polepole. Ni wajibu wetu kama wabunge kufuatilia miradi hii kuhakikisha kuwa imekamilika,” akasema.

“Kuna utaratibu ambao unapaswa kufuatwa kabla ya mwakandarasi kuanza kazi. Kiongozi wa hadhi ya Naibu Rais hawezi kuanzisha miradi ambayo haijatengewa fedha,” akaeleza Bw Osoro.

Suala la kukwama kwa miradi ya serikali katika kaunti ya Kisii lilichipuza juzi Rais Kenyatta alipozuru eneo hilo majuzi wakati viongozi walipomtaka Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati ili miradi hiyo ikamilishwe, wakisema hilo lisipofanyika wananchi watawalaumu.

Naye Mbunge wa Lugari katika Kaunti ya Kakamega, Ayub Savula amelalamika kuwa miradi iliyozinduliwa na Dkt Ruto katika eneo bunge hilo tangu 2015 imekwama.

“Naibu Rais alizindua mradi wa ujenzi wa chuo cha kiufundi katika eneo la Chevaywa mnamo Julai 2015. Lkini Sh100 milioni alizosema zilitengewa mradi huo hazijatolewa mpaka sasa. Juhudi zangu za kushinikiza kutolewa kwa fedha hizo hazijafua dafu,” Bw Savula akasema.

WAANDISHI WETU: CHARLES WASONGA, ERIC WAINAINA, GRACE GITAU, GEORGE MUNENE, VIVERE NANDIEMO na RUTH MBULA