Habari

MKASA WA GIKOMBA: Moto uliwashwa makusudi, wadai wafanyabiashara

June 28th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

MIVUTANO kuhusu ardhi na ushindani wa kibiashara ndizo sababu kuu zinazodaiwa kupelekea vifo vya watu 15  kwenye moto uliotokea katika soko la Gikomba, Nairobi usiku wa kuamkia Alhamisi.

Tukio hilo ndilo mbaya zaidi kuwahi kusababisha maafa makubwa kwenye misururu ya moto ambayo huzuka katika soko hilo maarufu mara kwa mara. Kwenye visa vya awali, mali ya thamani kubwa imekuwa ikiharibiwa, lakini kwenye moto wa jana maisha ya wengi yaliangamia.

Wengi wa waathiriwa hao walifariki wakiwa majumbani mwao, kwani walikuwa wangali wamelala.

Mengi ya makazi yaliyo karibu yalikuwa yamechomeka kabisa, yakionyesha ukubwa wa moto huo.

“Watu wengi wakikuwa bado usingizini, ikizingatiwa kwamba moto ulianza wakiwa washalala. Ilikuwa vigumu kuwaamsha,” akasema Ibrahim Njenga, aliyekuwa miongoni mwa watu wa kwanza kuanza harakati za uokozi.

Wafanyabiashara na wakazi wa mitaa inayopakana na soko hilo walielezea kwamba kumekuwa na taharuki za ushindani wa kibiashara katika soko hilo.

Ndimi za moto zililamba magorofa ambamo wakazi huishi. Picha/ Anthony Omuya

“Tunashuku moto huu uliwashwa kimakusudi. Hii ni njama inayoendeshwa na washindani wetu wa kibiashara. Wamekuwa wakiendesha njama hizo kwa kuwatumia walinzi ambao tumewaajiri ili kutulindia biashara zetu,” akasema Bw Samuel Kahuti, ambaye alisema alipoteza mali ya zaidi ya Sh1.6 milioni.

Kulingana naye, kuna maswali mengi yanayoandama kisa hicho, kwani baadhi ya walinzi walikataa kuwaarifu hata baada ya moto huo kuanza.

Baadhi ya wafanyabiashara wanaamini kwamba walinzi wao walitumika kimakusudi na mahasimu wao kuwasha moto huo.

“Mbona walikaa kwa hadi saa mbili tangu moto huo kuanza ndipo wakatueleza? Mbona baadhi yao walitoroka baada ya moto huo kuanza?” akashangaa.

Bw Mwangi Nduhiu, ambaye ni mmiliki wa duka la kuuzia vifaa vya ujenzi pia alitoa kauli kama hiyo, akidai wanyakuzi ambao wamekuwa wakimezea mate ardhi ya soko hilo ndio waliohusika.

Kulingana naye, kuna mzozo wa ardhi kuhusu eneo husika, hivyo kuna uwezekano kwamba wale wanaolimezea mate wanataka kutumia njia zozote ili kulipata.

Wakazi walijaribu kuuzima moto huo lakini ukawa umeharibu mali nyingi. Picha/ Anthony Omuya

“Soko hili nzima linaandamwa na utata. Kuna watu wanaotaka kulinyakua kutoka kwa walio na biashara zao, hivyo wamekuwa wakitumia njia zozote kuwatishia wanaoendesha biashara zao kihalali,” akasema Bw Mbuthia.

Moto huo unadaiwa kuanza saa sita za usiku katika kituo kimoja cha kuuzia mbao na kusambaa hadi katika makazi ya watu na vibanda vilivyo karibu.

Bw Daniel Otivi, ambaye alimiliki kibanda katika eneo lililoathirika alisema kuwa kuna taharuki za kikabila ambazo zimekuwepo kwa muda mrefu, hivyo “hawajashtushwa” na kisa hicho.

“Tiba kuu ya mzozo huu ni ugavi upya wa mpangilio wa soko, kwani tutaendelea kushuhudia matukio hayo ikiwa utathmini mpya hautafanywa,” akasema Bw Otivi, ambaye alisema alipoteza mashine ya Sh50,000 ya kushona nguo kwenye mkasa huo.

Baadhi ya watu wanadai kwamba jamii moja “imependelewa” katika ugavi wa maeneo ya kibiashara, hivyo lazima “wajitetee kwa kila namna.”

“Matukio haya ni ishara ya kutotosheka kwa jamii moja. Lazima ugavi mpya wa maeneo ya kibiashara ufanywe ili kurejesha hali ya amani,” akasema mfanyabiashara mmoja ambaye hakutaka kutajwa.