HabariSiasa

Mlima Kenya wasilazimishwe kumpigia Ruto kura 2022 – Wakalenjin

February 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na ONYANGO K’ONYANGO

BARAZA la Wazee wa Jamii ya Wakalenjin (Myoot) limetaka wapiga-kura wa eneo la Mlima Kenya wasilazimishwe kumpigia kura Naibu Rais Dkt William Ruto ili kumrithi Rais Uhuru Kenyatta hapo 2022.

Wazee hao katika mahojiano na Taifa Leo hapo Alhamisi walisema kuwa Rais Kenyatta na Dkt Ruto hawakutia saini mkataba wowote, hivyo wakazi wa Mlima Kenya wako huru kuchagua kiongozi yeyote wanayempenda.

Mwenyekiti wa Myoot, Bw John Seii, ambaye pia ni mjumbe wa Jopokazi la Mpango wa Maridhiano (BBI), hata hivyo, alisema kuwa jamii ya Agikuyu inaweza kuonyesha urafiki kwa kuunga mkono Dkt Ruto.

“Lakini rafiki zetu wa Mlima Kenya wakiona kwamba hawataki Dkt Ruto kumrithi Rais Kenyatta ambaye tulimpigia kura nyingi 2017 na 2013, basi tutakubali kwani siasa zinabadilika kila uchao,” akasema Bw Seii.

“Wana haki ya kumpigia kura kiongozi yeyote wanayehisi atashughulikia maslahi yao kwani hiyo ndiyo demokrasia,” akaongezea.

Lakini wandani wa Naibu Rais wanashikilia kuwa eneo la Mlima Kenya linafaa ‘kurudisha mkono’ kwa kumuunga Dkt Ruto katika uchaguzi mkuu ujao.

David Chepsiror, mjumbe wa baraza la Myoot, alisema kuwa eneo la Bonde la Ufa lina viongozi wawili ambao wamehitimu kuongoza nchi hii.

Alisema mbali na Dkt Ruto, Seneta wa Baringo, Bw Gideon Moi pia anatosha kuwa rais wa Kenya baada ya kukabidhiwa rungu la Nyayo la Mzee Daniel arap Moi.

Alisema Fimbo ya Nyayo imemfanya Bw Gideon Moi kuwa na nguvu nyingi katika siasa za Bonde la Ufa.

“Seneta wa Baringo sasa anaweza kuwania kiti chochote anachotaka. Hiyo pia inamaanisha kuwa chama cha Kanu hakijafa,” akasema Bw Chepsiror.

Lakini wandani wa Dkt Ruto wanasisitiza kuwa hawatakubali mwanasiasa yeyote kuhujumu juhudi za Naibu wa Rais kuingia ikulu 2022.

“Wakati umefika kwa Rais Kenyatta kutangaza msimamo wake wazi. Tungali tunashikilia ahadi ya Rais Kenyatta aliyotoa 2013 kuwa angeongoza kwa miaka 10 na kisha amwachie Dkt Ruto aongoze kwa miaka 10 mingine,” akasema mbunge wa Endebess, Robert Pukose.

Bw Pukose alidai kuwa kiongozi wa ODM Raila Odinga amekuwa akimpotosha Rais Kenyatta kwa kumpatia ushauri usiofaa ili amtelekeze Dkt Ruto.