Habari

Mwenye lori lililotumbukia baharini likiwa feri alipwa Sh6.1 milioni

Na PHILIP MUYANGA April 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MFANYABIASHARA mmoja ambaye lori lake lilitumbukia katika Bahari Hindi miaka 15 iliyopita katika kivukio cha feri amelipwa fidia ya Sh6.1 milioni.

Mahakama ya Rufaa iliwapata na makosa wahudumu wa feri hiyo, haswa nahodha na aliyekuwa akishughulikia kufunguliwa na kufungwa kwa rampu, ambaye alikuwa na wajibu wa kuhakikisha kuwa magari yameingia ndani ya feri salama kabla ya safari ya kuvuka bahari kuanza.

Bw Daniel Kiiru wa kampuni ya Kinamba General Suppliers and Transport, alikuwa ameshtaki Huduma za Feri (KFS) na Mamlaka ya Bandari Nchini (KPA), akidai kuwa feri hiyo iliondoka mapema kabla ya gari lake kuingia kwenye chombo hicho, na kuifanya kutumbukia baharini.

Hapo awali, mahakama kuu ilikuwa imetupilia mbali kesi ya Bw Kiiru, ila akakata rufaa. Mnamo Aprili 11, mahakama ya rufaa ilitoa uamuzi kumpendelea Bw Kiiru, ikisema kuwa pande zote husika zililaumiwa kwa kiwango fulani.

Mahakama iliamua kuwa asilimia 70 ya ajali hiyo ilisababishwa na wahudumu wa feri huku asilimia 30 ikiwa ni makosa ya dereva wa Bw Kiiru.

Majaji Agnes Murgor, Kibaya Laibuta na Grace Ngenye-Macharia walieleza kuwa nahodha angesubiri kupewa taarifa na mwenye wajibu wa kufunga rampu hiyo kabla ya kuondoka, na dereva aliihitaji maarifa zaidi ya kuendesha gari hilo zito akiliingiza ndani ya feri.

“Dereva wa mlalamishi alipaswa kuwa na ujuzi wa kutosha wa kumsaidia kuendesha gari hilo na kuliingiza kwenye feri na kuijaza feri kama kawaida bila shida yoyote,” wakasema majaji hao.

Walieleza pia kuwa,huenda mawasiliano baina ya nahodha na aliyeshughulikia rampu, yangezuia ajali hiyo.

“Mwendeshaji au nahodha hakupaswa kuondoka tu kwa fikra zake. Hakuna ushahidi uliotolewa kuonyesha kuwa nahodha alijulishwa kwamba kulikuwa na gari lililokuwa likijaribu kuingia ndani ya feri wakati wa kung’oa nanga.”

Aidha, mahakama ilisema kuwa kulikuwa na uwezekano wa gari hilo kuwa na hitilafu, kwani ilipata shida wakati wa kuingia ndani ya feri.

Ilieleza kuwa ili gari liingie ndani ya feri, lililazimika kupita kwenye mteremko na kwa hivyo halingetatizika kuingia ndani ya feri.

“Badala yake, badaa ya majaribio kadhaa, sehemu ya lori haikuweza kuingia ndani ya feri, hii lazima ilisababishwa na hitilafu katika gari husika,” wakaamua majaji Murgor, Laibuta na Ngenye Macharia.

Licha ya hiyo, walisema kuwa haikuwa sababu ya feri kuondoka mapema.

KPA na KFS, waliowakilishwa na wakili Farida Jadi, walipinga rufaa hiyo, wakisema mfanyabiashara huyo alikuwa tayari amefidiwa na alikosa kuonyesha hasara aliyopata.

Licha ya hayo, mahakama haikukubaliana naye na kutoa uamuzi uliompendelea Bw Kiiru.

Walieleza pia kuwa, huenda mawasiliano baina ya nahodha na aliyeshughulikia rampu, yangezuia ajali hiyo.

Aidha, mahakama ilisema kuwa licha ya uwezekano kuwa gari hilo lilikuwa na hitilafu, si sababu ya feri hiyo kuondoka mapema.