Mzee, 83, apata makao mapya kijijini Nyamang'ara
Na LAWRENCE ONGARO
MZEE mmoja ambaye iliwahi kuripotiwa kwamba alitelekezwa na familia yake katika kijiji cha Nyamang’ara, Gatundu Kaskazini, amepata msaada na kujengewa nyumba mpya.
Bw Francis Kahura, 83, aliyekuwa akiishi msituni alipata afueni wakati mbunge wa eneo hilo Bi Anne Wanjiku Kibe, aliingilia kati na kumjengea nyumba mpya.
“Mimi nimeishi msituni kwa muda mrefu baada ya jamaa zangu ‘kunitupa’, huku wakikosa kunitunza ipasavyo. Sasa nina furaha kuu kuona ya kwamba Bi Kibe amenisaidia pakubwa,” alisema Bw Kahura mnamo Jumatatu huku akitabasamu.
Bi Kibe ambaye alizuru kujionea nyumba hiyo mpya iliyofunguliwa siku chache zilizopita alimkabidhi blanketi, godoro, na matandiko mengine muhimu kumsaidia mkongwe huyo kujifunika vilivyo.
“Mimi furaha yangu ni kuona ya kwamba mkongwe huyu aliyetelekezwa na jamaa zake amerejea katika maisha mazuri. Nitahakikisha kila siku anakula vizuri na anatunzwa kwa njia inayostahili,” alisema Bi Kibe, na kuongeza, “Ningetaka nyinyi wakazi wa hapa pia muonyeshe moyo wa huruma kwa kumtunza mkongwe huyu ambaye mnamwona umri wake umesonga sana.
Ilidaiwa ya kwamba hapo awali mkongwe huyo alipokuwa msituni wahuni walimvamia na kumkata kwa panga ambapo alijeruhiwa vibaya, huku akipelekwa hospitalini.
Baada ya hapo ndipo ujumbe ulipowasilishwa kwa mbunge wake Bi Kibe ambaye bila kupoteza muda aliamua kumjengea nyumba ya chumba kimoja.
Makao maalumu
Wakazi wa kijiji hicho walimpongeza Bi Kibe kwa kuchukua hatua hiyo ya dharura na kuhakikisha mzee huyo mkongwe anapata makao maalumu.
“Sisi tumepongeza hatua uliyochukua ya kumhifadhi mkongwe huyu katika nyumba nzuri ya kisasa. Hiyo ni hatua nzuri ya kuonyesha jinsi unavyowatambua wasiojiweza, tunakushukuru zaidi,” alisema Paul Njuguna ambaye ni mkazi wa kijiji cha Nyamang’ara.
Familia za eneo hilo zimehimizwa kuwalinda wakongwe kwani hiyo ni baraka hata kwa Mwenyezi Mungu.
“Kila mara nitakuwa nikizuru eneo hili ili kumjulia hali mzee huyu ambaye ninamwita babu yangu na mzazi pia. Kwa hivyo jukumu hili la kumchunga mzee wetu liwe letu sote na tutafanikiwa,” alisema Bi Kibe.