KAUNTI ya Nairobi iliripoti dhuluma nyingi dhidi ya wanafunzi, ikiwemo Dhuluma za Kijinsia (GBV), kuhangaishwa mitandaoni na dhuluma nyingine kwa mujibu wa Ripoti ya Tume ya Kitaifa ya Jinsia na Usawa (NGEC).

Kwa mujibu wa ripoti hiyo asilimia 66.7 za shule za Nairobi ziliripoti kuhusu angalau mwanafunzi mmoja kudhulumiwa.

Kupigwa na dhuluma za kimapenzi ziliathiri wavulana na wasichana.

Kitui ilifuata Nairobi kwenye visa vya dhuluma dhidi ya wanafunzi kwa asilimia 36.4.

Isiolo iliongoza kati ya kaunti ambazo zina visa vingi vya kuwafanyisha wanafunzi kazi za suluhu huku wavulana wakiathirika kwa asilimia 50 huku wasichana wanaofanya kazi za nyumbani wakiwa asilimia 40.

Laikipia na Baringo zilifuata kwa idadi ya wavulana wanaofanyishwa kazi za sulubu kwa asilimia 36.

Meru na Baringo pia zilikuwa na idadi ya juu ya wasichana wanaofanya kazi za nyumbani kwa asilimia 20 na 18 mtawalia.

Visa vya ukeketezaji bado vimeshamiri Baringo (asilimia 27.3), Garissa (asilimia 27.3) kisha Narok kwa asilimia 21.4.  Hii inaonyesha kuwa kaunti za wafugaji bado zina kazi kutokomeza tabia hii.

Kitui, Makueni, Kwale, Turkana, Pokot Magharibi, Samburu, Kilifi na Nairobi ni kaunti ambazo hazikuwa na kisa chochote cha ukeketaji.