Nairobi yaongoza maambukizi, Mombasa kwa vifo
Na JUMA NAMLOLA
KAUNTI ya Nairobi inaongoza kwa idadi ya maambukizi ya virusi vya corona huku Mombasa ikiongoza kwa watu walioaga dunia kutokana na ugonjwa wa Covid-19.
Wizara ya Afya ilitangaza kwamba kati ya visa 963 vilivyoripotiwa kufikia Jumanne, Nairobi ina 470.
Aidha, kati ya vifo 50, Mombasa imechangia 27.
Waziri wa Afya, Bw Mutahi Kagwe aliyetokea kwa mara ya kwanza katika kipindi cha wiki nzima, alisema jana kuwa, kati ya watu 1,933 waliopimwa kuna wanaume 32 na wanawake 19 waliambukizwa.
“Kufikia leo (jana Jumanne), tumepima jumla ya watu 46,784. Tunafurahi kuwa watu wengine 22 wameruhusiwa kurudi nyumbani, na kufanya idadi ya waliopona kuwa 358,” akasema.
Orodha ya kaunti kumi zinazoongoza kwa maambukizi inaonyesha Mombasa inachukua nafasi ya pili kwa visa 331. Maambukizi katika kaunti nyingine ni; Kajiado (43), Mandera (18), Kiambu (17) na Wajir (16). Migori ina visa 14, Kilifi (10), Kwale (7) huku Kitui na TaitaTaveta zikiwa na visa vitano kila moja katika nafasi ya kumi.
Takwimu zinaonyesha kwamba watu wa umri wa kati ya miaka 20 na 39 ndio walioambukizwa zaidi.
Waziri Kagwe alisema kati ya vifo 50, Mombasa kuna watu 27 waliokufa ikifuatwa na Nairobi (20) huku Siaya, Bomet na Kiambu zikiwa na kisa kimoja kimoja.
Alionya kwamba vifo hivyo vinaweza kusababisha maambukizi zaidi iwapo vitatokea nyumbani.
“Idadi kubwa ya waliofariki Mombasa walikuwa nyumbani. Hii inahatarisha maisha ya watu wengi zaidi, ikizingatiwa kuwa huenda watu waliwazika bila kuzingatia kanuni za usalama,” alieleza.
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw Adan Mohamed alionekana kupuuza mzozo uliopo kati ya Kenya na Tanzania kuhusu mipaka yao.
Alisema, kinyume na taarifa kuwa Tanzania imezuia madereva wa matrela kutoka Kenya, magari hayo yanaendelea kusafiri kati ya pande zote mbili.
Siku ya Jumatatu, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Bw Martine Shigela, alitoa maagizo kwa walinzi wa mpakani eneo la Horohoro, kwamba wasiwaruhusu madereva kutoka Kenya kuingia Tanzania.
Bw Shigela alisema malori pekee kutoka Kenya yatakayoruhusiwa ni yale yanayopeleka mizigo katika mataifa ya Malawi, Rwanda, Msumbiji na kadhalika.
Lakini Jumanne Bw Mohamed alisema hali iko shwari na madereva wa Kenya wanaendelea kupimwa virusi vya corona na kuvuka mpaka huo.