Habari

Nchuri Ncheke tayari kuomba msamaha kwa niaba ya Kithure Kindiki

May 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

CHARLES WASONGA na ALEX NJERU

WAZEE wa jamii ya Ameru – Njuri Ncheke – wanasema wako tayari ‘kupiga magoti’ kwa niaba ya mtoto wao, Profesa Kithure Kindiki, ikiwa itabainika alimkosea mtu yeyote.

Walisema hayo saa chache baada ya Spika wa Seneti Kenneth Lusaka kuitisha kikao maalum cha bunge hilo kesho Ijumaa kujadili na kupigia kura hoja ya kumvua Profesa Kindiki wadhifa wa Naibu Spika.

Lakini akiongea na Taifa Leo, Mwenyekiti wa Wazee hao Linus Kathera alisema Jumatano wanauliza wahusika kujua makosa ya Seneta huyo wa Tharaka Nithi ili waweze kuingilia kati kabla ya hoja hiyo kujadiliwa na kuamuliwa.

“Profesa Kindiki ni mwana wetu na tunashauriana na viongozi wahusika ili tufahamishwe makosa ambayo alifanya kuchochea kupokonywa kwake cheo cha Naibu Spika wa Seneti,” Bw Kathera akasema.

Alisema ikiwa watagundua hatua hiyo inachochewa na siasa wazee watajua namna ya kufuatilia suala hili kuhakikisha kuwa “mwana wao” hadhulumiwi.

Bw Kathera alisema wajibu wa Baraza la Wazee la Njuri Ncheke ni kukinga wana wa jamii ya Ameru na kamwe hawatanyamaza wakati ambapo mmoja wa mwana wao anayeshikilia wadhifa wa juu serikali anadhulumiwa.

Aliongeza kuwa endapo Profesa Kindiki ametenda kosa lolote wako tayari kuomba msamaha kulingana na mila za Ameru kwa yule aliyekosewa.

Bw Kathera alisema wazee hao hawajafurahishwa na mivutano ya kisiasa inayoendelea katika ngazi ya kitaifa ya chama cha Jubilee.

“Tuko tayari kuingilia kati na kukomesha migogoro hii ya kisiasa ambayo imeshamiri katika ngazi ya kitaifa ndani ya Jubilee na hata serikalini,” akasema.

Na katika ilani iliyochapishwa katika toleo la Gazeti Rasmi la Serikali nambari 3646, Spika Lusaka alisema shughuli ya kujadili hoja hiyo na kuipigia kura ndiyo itakuwa ya kipekee wakati wa kikao hicho maalum.

“Ilani inatolewa kwa maseneta wote kwamba kwa mujibu wa sheria ya seneti nambari 30, baada ya kupokea ombi kutoka kwa Kiongozi wa Wengi, na kuungwa mkono na idadi tosha ya maseneta, nimeitisha kikao maalum cha Seneti mnamo Ijumaa, Mei 22, 2020,” akasema.

“Nimeitisha kikao hicho kwa ajili ya kujadiliwa na kuamuliwa kwa hoja ya kumwondoa ofisini Naibu Spika wa Bunge la Seneti Kithure Kindiki,” akaongeza.

Kikao hicho kitafanyika katika Ukumbi wa Mijadala ya Seneti saa nane na nusu alasiri hadi shughuli za siku hiyo zitakapokamilishwa.

Mnamo Jumanne, Kiranja wa Wengi Irungu Kang’ata aliwasilisha rasmi ilani ya hoja ya kumvua Profesa Kindiki wadhifa wake.

Japo hakutaja sababu zilizochangia hatua hiyo, awali alikuwa ameambia wanahabari kwamba Kindiki anaondolewa kwa kususia mkutano wa maseneta wa Jubilee ulioongozwa na Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi wiki jana.

Duru ziliambia Taifa Leo kwamba tayari maseneta 51 wameunga mkono hoja hiyo; ishara kwamba hatima ya Profesa Kindiki tayari imeamuliwa.