Habari

Ni kweli Raila aliugua lakini anaendelea kupata nafuu India, asema Oburu

Na RUSHDIE OUDIA October 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SENETA wa Siaya, Dkt Oburu Oginga, amethibitisha kuwa ndugu yake mdogo, aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, alikuwa mgonjwa kwa muda, lakini sasa anaendelea kupata nafuu nchini India.

Kauli yake inajiri siku chache baada ya uvumi na taarifa zinazokinzana kusambaa kuhusu hali ya kiafya ya Kiongozi wa chama cha ODM.

Akizungumza na wanahabari akiwa Ugunja na pia kwenye kipindi cha asubuhi katika redio ya lugha ya mama, Radio Nam Lolwe, Dkt Oginga alieleza kuwa ugonjwa huo haukuwa wa kutishia maisha.

“Raila, kama binadamu yeyote, alipata matatizo madogo ya kiafya siku chache zilizopita, lakini kwa sasa anaendelea vizuri. Alisafiri kwenda India kwa uchunguzi wa kiafya na sasa anapumzika,” alisema Dkt Oginga, ambaye pia ni msemaji wa familia ya Odinga.

Hata hivyo, kauli yake inakinzana na ile ya mke wa Raila, Mama Ida Odinga, ambaye hivi majuzi alikanusha madai kuwa mumewe ni mgonjwa, akieleza kuwa amechukua likizo fupi kutoka  siasa.

“Kama mtu ninayeishi naye kila siku, naifahamu afya yake vyema kuliko mtu mwingine yeyote. Haieleweki ni vipi mtu asiyeishi naye anaweza kudai anajua hali yake ya afya kuliko mimi. Ninachowaambia ndicho ukweli,” alisema Mama Ida.

Aidha, msemaji wa Raila, Dennis Onyango, na timu yake walikuwa tayari wamekanusha madai hayo, wakisema ni propaganda za kisiasa zilizoenezwa na wapinzani.

Ingawa Bw Odinga kwa kawaida huwa wazi kuhusu hali yake ya afya, Dkt Oginga alisema kuwa lazima Raila aarifu  umma kila mara kuhusu hali yake kwa kuwa yeye si rais.

“Raila si rais ambaye afya yake lazima ijulikane hadharani kila mara, hata kwa matatizo madogo kama haya. Hatukukusudia kuzungumzia suala hili hadharani, lakini kutokana na uvumi uliokuwa umeenea, tuliamua kutoa ufafanuzi,” alisema Dkt Oginga.

Alisisitiza kuwa Bw Odinga atarejea nchini hivi karibuni baada ya kupata nafuu kamili.