NMG yamwomboleza mhariri wa The East African
Na AGGREY MUTAMBO
KAMPUNI ya Nation Media Group (NMG) kwa mara nyingine inaomboleza kifo cha mwanahabari katika kipindi kisichozidi mwezi mmoja.
Mhariri wa gazeti la The East African Bi Christine Omulando aliyekuwa na umri wa miaka 46, alifariki kufuatia ajali iliyotokea katika mzunguko wa Khoja, jijini Nairobi hapo Machi 16.
Kulingana na ripoti ya polisi, mwanahabari huyo pamoja na wapita njia wengine waliligongwa na matatu iliyokosa udhibiti na kutoka barabarani kabla ya basi ndogo kumkanyaga.
“Bi Omulando alifariki papo hapo baada ya kugongwa na basi ndogo,” ilisema ripoti.
Mwili wake ulipelekwa kwenye nyumba ya kuhifadhia maiti jijini na wapita njia waliohusika wakakimbizwa katika hospitali kuu ya Kenyatta.
Mwanahabari huyo aliripotiwa kupotea Jumatano baada ya familia na marafiki kushindwa kumfikia kwa njia ya simu.
Asubuhi hiyo, alikuwa amefika kazini kisha baadaye akaondoka kwenda kula maankuli.
Hiki ni kisa cha pili, huku wanahabari wa NMG bado wakimwomboleza aliyekuwa mhariri wa video katika runinga ya NTV Raphael Nzioki.
Polisi walisema kuwa marehemu aligongwa kimaksudi na gari kwenye njia panda katika mtaa wa Kenyatta Avenue na Kimathi Street.
Madereva waliohusika katika visa vyote hivyo viwili tayari wamekamatwa.