HabariSiasa

ODM yaanza kujipanga kwa uchaguzi wa 2022

May 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

CHAMA cha ODM kimeanza kuweka mikakati ya kujiandaa kwa Uchaguzi Mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika 2022.

Baraza Kuu la Kitaifa la chama hicho (NEC) kinachoongozwa na Bw Raila Odinga kiliagiza afisi simamizi ya chama chini ya Katibu Mkuu, Bw Edwin Sifuna ijiandaye kwa uchaguzi wa maafisa wa mashinani utakaofanyika mwaka ujao.

Kwa kawaida, uchaguzi wa maafisa mashinani huwa na umuhimu mkubwa kwa maandalizi ya chaguzi kuu katika chama chochote kilicho na uungwaji mkubwa nchini.

Kupitia taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari, Msemaji wa ODM, Bw Philip Etale alisema katiba ya chama huhitaji uchaguzi wa maafisa wa chama mashinani kufanyika kila baada ya miaka mitano.

Taarifa hiyo ilitolewa baada ya mkutano wa NEC Jumatatu uliohudhuriwa pia na Bw Odinga ukiongozwa na Mwenyekiti wa Chama, Bw John Mbadi.

Katika mkutano huo, NEC iliunda kikundi cha wanachama watatu kuchanganua ripoti iliyotolewa na jopokazi ambalo lilikuwa limeteuliwa mwaka uliopita kutafuta mbinu bora zaidi ya kufanya uteuzi wa wagombeaji viti chamani humo.

Jopokazi hilo lilisimamiwa na Bi Catherine Mumma huku wanachama wake wakiwa Seneta Maalumu aliye pia Mwenyekiti wa Bodi ya Uchaguzi Kitaifa katika ODM, Bi Judith Pareno, Mbunge wa Nyando, Bw Jared Okello na Mkurugenzi Mkuu wa ODM, Bw Oduor Ong’wen.

“Jopokazi lilikuwa limeundwa ili kutathmini mbinu za uteuzi chamani na kutoa mapendekezo kuhusu mbinu bora zaidi zinazoweza kutumiwa. Ripoti ina mapendekezo mengi kuhusu muundo wa chama, sera zake na jinsi ya kufanya kura ya mchujo na uchaguzi wa maafisa wa mashinani miongoni mwa mapendekezo mengine,” akaeleza Bw Etale.

Lilikuwa limebuniwa kufuatia malalamishi mengi kutoka kwa baadhi ya wanachama kuhusu jinsi uteuzi wa wagombeaji umekuwa ukifanywa katika miaka iliyopita, wakati mwingi kura za mchujo zikisababisha hata umwagikaji damu na maafa.

Miongoni mwa malalamishi yaliyoibuka ni madai ya wanasiasa kutumia mbinu za ulaghai kupata vyeti vya ugombeaji katika ODM, hali ambayo imesababisha chama hicho kupoteza viti katika ngome zake za kisiasa wakati wanachama mashuhuri wanaonyimwa vyeti wanahamia vyama pinzani au kuamua kuwa wagombeaji huru.

Baadhi ya mapendekezo ambayo yamekuwa yakitolewa na wanachama ni kwamba, kusiwe na kura ya mchujo bali chama kipeane tikiti moja kwa moja kwa mgombeaji anayeonekana wazi kuwa maarufu na pia aliye mzalendo kwa chama.

Mwezi uliopita, mgombeaji ubunge katika uchaguzi mdogo wa Ugenya, Kaunti ya Siaya kwa tikiti ya ODM, Bw Christopher Karani alishindwa na Bw David Ochieng ambaye aliwania kwa chama cha Movement for Democracy and Growth (MDG).

Ngome nyingine za kisiasa ambapo ODM ilishindwa kwa ubunge ni Kisumu Mashariki ambapo Bw Shakeel Shabbir alishinda licha ya kuwa mgombeaji huru, Kisumu Magharibi ambapo Bw Olago Aluoch alishinda kupitia Ford Kenya, Nyali (Kaunti ya Mombasa) ambapo Bw Mohamed Ali alishinda kwa kuwa mgombeaji huru.