Habari

OneTam: Hauwezi kutufikisha Singapore labda Somalia, Gachagua aambia Ruto

Na MWANGI MUIRURI November 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KIONGOZI wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP), Rigathi Gachagua, amekosoa vikali hotuba ya Rais kuhusu Hali ya Taifa, akidai kuwa ilikuwa maneno matupu yasiyoonyesha mwelekeo halisi wa taifa.

Akimshambulia Rais moja kwa moja, Bw Gachagua alisema kuwa madai ya Rais Ruto kuwa anaelekeza Kenya kufikia hadhi ya “Singapore” ni porojo.

Kwa hamaki, aliongeza: “Unasema unatufanya kuwa kama Singapore, lakini kwa kweli unaturudisha nyuma hadi 1963, kwenye umaskini, maradhi na ukandamizaji. Kufikia uchaguzi ujao tutakuwa Somalia.”

Bw Gachagua alisema serikali ya Rais Ruto imejawa na ufisadi, ukandamizaji wa haki, na ukosefu wa uwajibikaji.

Alipuuzilia mbali mpango wa Rais wa kuwekeza Sh5 trilioni katika elimu, uzalishaji, umeme na ujenzi wa barabara, akisema kuwa ni kuficha ufisadi uliopangwa.

Akirejelea mpango wa makato ya ushuru wa Nyumba Gachagua alisema Rais alipaswa kutangazia taifa kuondolewa mara moja na kurejeshea wafanyakazi pesa zao “Singapore ina mshahara wa wastani wa Sh700,000 kwa mwezi.

Wetu ni Sh70,000 halafu mnatukata ushuru wa zaidi ya nusu ya mshahara wenyewe. Huo si mwelekeo wa kutufanya kuwa kama Singapore.”

Akiendelea kukosoa utawala wa Ruto, Bw Gachagua alidai kuwa Ajenda Nne Kuu za Rais mstaafu Uhuru Kenyatta na miradi ya Ruwaza 2030 “zilibomolewa” na Rais Ruto ili kufungua mianya ya ufisadi.

“Hustler Fund si hadithi ya mafanikio. Ni mkopo mdogo usiomaliza umaskini, bali kuongezea maskini madeni,” alisema.

Kuhusu Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), Gachagua aliitaja kama “ulaghai mkubwa unaowanufaisha wachache,” akisema Wakenya milioni 27 waliojiandikisha bado hawajui manufaa yake.

Alidai pia kuwa ajira za walimu 76,000 alizotangaza Rais hazikutolewa kwa uwazi, akisema baadhi ya barua “zilidaiwa kugawiwa wanasiasa waaminifu Ikulu.”

Akikosoa mipango ya miundombinu aliyotangaza Rais, Bw Gachagua alishangaa atatoa wapi fedha za kujenga kilomita 2,500 za barabara za njia mbili, kilomita 28,000 za lami, na kupanua reli ya SGR hadi Kisumu na Malaba.

“Fedha chache tunazokusanya zinapotelea kuhonga wapiga kura. Hiyo ndiyo mnaita safari ya kuwa kama Singapore?” alihoji.

Kiongozi huyo alisema Kenya inahitaji taasisi imara, uadilifu wa bajeti, na usawa kwa raia wote na “sio uongo na burudani ya kisiasa.”

Alidai kuwa Rais Ruto amekuwa akituma wajumbe kwake warudiane.

“Rais Ruto anatuma wajumbe kwangu. Lakini samahani, uliniacha nikiwa maskini na dhaifu. Sasa nimepata nguvu na mali. Siwezi kukurudia. Hata ‘watoto’ tuliokuwa nao, Mlima Kenya, hawakutambui tena,” alisema.

Bw Gachagua alisisitiza kuwa hahitaji tena kuungano na Rais Ruto. “Uliniacha nikiwa dhaifu, sasa umenirudia nikiwa na nguvu. Pole sana, mimi si wa kurudi nyuma.”