Onyo serikali iache kukopa kiholela
MDHIBITI wa Bajeti (CoB) Margaret Nyakang’o ameonya serikali dhidi ya kukopa kupita kiasi kwa miradi ya maendeleo isiyo na faida za moja kwa moja za kiuchumi au kijamii, huku akieleza kuwa Sh507.98 bilioni zilitumika kulipa madeni katika miezi mitatu ya kwanza ya mwaka wa kifedha wa 2025/26.
Katika ripoti yake ya utekelezaji wa bajeti ya kitaifa kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha, Bi Nyakang’o alisema ongezeko la ukopaji ili kufadhili bajeti ya Sh4.69 trilioni linaendelea kubana nchi kifedha, hasa pale mikopo inapochukuliwa kwa miradi isiyoleta manufaa yanayopimika kwa wananchi.
Kiasi cha malipo ya madeni katika kipindi hicho kinawakilisha asilimia 27 ya makadirio yaliyorekebishwa, ikilinganishwa na Sh325.52 bilioni (asilimia 17) zilizolipwa katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha wa 2024/25.
Kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti wa Bajeti, ongezeko hilo linatokana hasa na malipo ya kiasi halisi kilichokopwa ndani na ya nje, ambayo yalifikia Sh251.80 bilioni, kutoka Sh95.54 bilioni katika kipindi kama hicho mwaka uliopita.
“Ili kuboresha athari za kifedha na kuhakikisha uendelevu wa deni, ukopaji unapaswa kujitokeza kikamilifu katika miradi ya maendeleo yenye faida za kiuchumi na kijamii zinazoweza kupimika,” alisema Bi Nyakang’o.
Kwa mwaka huu wa fedha, serikali imetenga Sh1.90 trilioni kulipa deni la umma ikilinganishwa na Sh1.74 trilioni zilizotengwa mwaka wa 2024/25.
Kati ya fedha hizo Sh1.10 trilioni zilitengwa kwa riba.
Katika miezi mitatu ya kwanza ya 2025/26, serikali ililipa Sh213.09 bilioni kwa deni la nje, likijumuisha Sh141.10 bilioni kwa kiasi kilichokopwa na Sh71.68 bilioni kama riba.
Aidha, Sh294.89 bilioni zililipwa kwa deni la ndani, zikiwemo Sh110.70 bilioni kiasi kilichokopwa na Sh184.20 bilioni za riba.
Mdhibiti wa Bajeti alisema deni la umma linaloongezeka limekuwa likimeza sehemu kubwa ya mapato ya ndani, hali inayobana matumizi ya kawaida na ya maendeleo.
Hii imelazimu serikali kukimbilia mikopo ya kibiashara kulipa mishahara, miradi ya maendeleo na hata kulipa madeni yenyewe.
“Matumizi ya kawaida yanapaswa kudhibitiwa kupitia uratibu wa matumizi, kuongeza ufanisi na kuimarisha udhibiti wa usimamizi wa fedha za umma,” alisema.
Ripoti inaonyesha deni la umma liliongezeka kwa asilimia mbili kutoka Sh11.80 trilioni kufikia Juni 30, 2025 hadi Sh12.04 trilioni kufikia Septemba 30, 2025.
Ingawa deni la nje lilipungua kwa asilimia mbili kutokana na malipo, deni la ndani liliongezeka kwa asilimia tano kutokana na kuongezeka kwa ukopaji wa ndani.
Kwa sasa, deni la nje ni Sh5.39 trilioni (asilimia 45) huku deni la ndani likiwa Sh6.65 trilioni (asilimia 55). Serikali inalenga kufadhili bajeti ya 2025/26 kupitia mapato ya kodi, mikopo ya ndani na ya nje, pamoja na misaada na mapato mengine ya ndani.