HabariSiasa

Polisi walimvunjia Sonko heshima Voi – Raila

December 9th, 2019 1 min read

NA CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga amekosoa namna ambavyo polisi walimkamata Gavana wa Nairobi Mike Sonko katika uwanja mdogo wa ndege wa Ikanga mjini Voi.

Akiongea na wanahabari wa Shirika la Habari la Nation (NMG) jijini Kigali, Rwanda, Bw Odinga alisema polisi walimkosea heshima na kumdhulumu Bw Sonko, bila sababu, kwa kutumia nguvu kupita kiasi wakati wa purukushani  iliyopelekea kukamatwa kwake.

“Ingawa maafisa wa polisi husika walikuwa na sababu ya iliyopelekea wao kumkamata kwa njia hiyo, nasema udhalimu kama huo haukuhitajika na haikupendeza,” akasema.

Bw Odinga ambaye pia ni Mjumbe Maalum wa Umoja wa Afrika (AU) kuhusu Miundo Msingi ni mmoja wa watu mashuhuri wanaohudhuria hafla ya Kusi Idea Festival ambayo ni sehemu ya maadhiminisha ya miaka 60 tangu kuasisi wa shirika la NMG.

Ijumaa, sinema ya aina yake ilitokea katika uwanja mdogo wa ndege wa Ikanga wakati Bw Sonko alipopambana na zaidi ya maa alikamatwa na zaidi ya maafisa wa polisi 200 walimvamia na kumtia pingu.

Katika kukurukakara hizo, zilizonaswa kwenye kanda ya video Sonko anaonekana akiwarushia mikono maafisa wa polisi huku akiwazomea kwa maneno makali katika hali ya kuzuia kutiwa mbaroni.

Hatimaye walimzidi nguvu na kumtia pingu na kulazimisha kuabiri helikopta ya polisi na kusafirishwa hadi Nairobi na kuzuiliwa katika afisi za Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).

Gavana Sonko alikamatwa saa chache baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DDP) Noordin Haji kutoa amri akamtwa pamoja na maafisa wengine na serikali ya kaunti ya Nairobi kuhusiana na sakata ya matumizi ya Sh357 milioni kupitia utoaji zabuni kinyume cha sheria.