Polisi wanyama waadhibiwe, kafyu ianze saa tatu – Dkt Aukot
VICTOR RABALLA NA FAUSTINE NGILA
KIONGOZI wa chama cha Thirdway Alliance Kenya Dkt Ekuru Aukot ameitaka serikali kuwachukulia hatua kali maafisa wa polisi waliokiuka haki za kibinadamu kwa kuwacharaza mijeledi Wakenya katika saa za kafyu.
Dkt Aukot amesema polisi walioonekana kwa picha na video wakiwapiga na kuwaumiza Wakenya kabla ya kafyu kuanza wanafaa kutambuliwa na kufikishwa mahakamani.
Ameitaka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kuchunguza visa hivyo na kuwafungulia mashataka polisi hao.
“Kupitia vitendo vyao vya kinyama, polisi hawa wanaeneza visuri vya corona ambavyo tunajaribu kuzuia kusambaa kwake,” amesema na kuongeza kuwa tayari Wakenya wanateseka na majanga mengine.
Kwenye barua aliyotumia Mkuu wa Polisi Bw Hillary Mutyambai hapo Jumapili, kiongozi huyo ambaye alitambua kazi ya polisi, aliwakosoa maafisa waliotumia nguvu kupita kiasi.
Pia, alimuomba Rais Uhuru Kenyatta kuongeza saa mbili kwa muda wa kafyu kuanza ili iwe ikianza saa tatu usiku kuwapa nafasi Wakenya kutafuta chakula cha usiku.