Polisi watetea udhalimu wao
Na LEONARD ONYANGO
IDARA ya Polisi imetetea maafisa wake wawili ambao walinaswa katika video wakimtesa na kumhamisha kwa nguvu mwanamke kutoka nyumba za polisi katika Kituo cha Buruburu, Nairobi.
Video hiyo iliyoonyesha mwanamke akifanyiwa ukatili ilichipuza mtandaoni Jumapili na kuzua ghadhabu miongoni mwa Wakenya katika mitandao ya kijamii.
Kulingana na Idara ya Polisi, mwanamke aliyekuwa akihamishwa kwa nguvu ni mke wa konstebo wa polisi aliyetambuliwa kwa jina la Charles Ochieng Adao anayedaiwa kuhepa kazi tangu Januari 1 na amekuwa akisakwa na polisi.
“Mwanamke huyo alipewa ilani ya kuondoka katika nyumba za polisi baada ya mumewe ambaye ni afisa wa polisi kukosa kufika kazini tangu Januari, mwaka huu,” ikasema taarifa ya polisi.
Idara hiyo ya usalama ilisema Bw Adao amekuwa akisakwa na polisi baada ya kupata kibali cha kumkamata mahakamani mnamo Januari 31, 2018.
Kulingana na taarifa hiyo, kufikia sasa afisa huyo hajulikani aliko.
Hata hivyo, inakiri kwamba mkewe amekuwa akiishi katika nyumba ya polisi katika kituo cha Buruburu.
Polisi walisema mkewe Adao alipewa ilani ya kuhama lakini akaruhusiwa kuendelea kuishi ili kuwezesha watoto kufunga shule katika muhula wa kwanza mwaka huu.
Katika video hiyo ambayo imekuwa ikisambazwa katika mitandao ya kijamii, mwanamke huyo anasikika akiwataka maafisa wa polisi wanaomhamisha kwa nguvu kutomtesa.
‘Mbona wanipiga bure?’
“Nimefanya nini? Unanipiga kwa nini…Haki nimekufanyia nini?’ alisikika akisema huku majirani wakipiga kamsa ya kuwataka maafisa hao kuachana naye.
Ripoti ambazo hazijathibitishwa zinaonyesha kuwa Bw Adao amekuwa akiugua maradhi ya kiakili na anatibiwa katika moja ya hospitali nchini.
Lakini idara ya polisi ilisema kuwa haijapata habari zozote kuhusiana na maradhi hayo na wala familia yake haijawahi kutoa taarifa kuhusiana na alipo.
“Idara ya Polisi haina taarifa kuhusiana na kulazwa hospitalini kwa Bw Adao na wala familia yake haijatoa ripoti kuhusiana na aliko afisa huyo wa polisi tangu alipotoweka Januari 2018. Mkewe amekuwa akitueleza kwamba hajui aliko mumewe,” ikasema taarifa ya polisi.
“Tumeanzisha uchunguzi ili kujua aliko afisa huyo na endapo atapatikana tutampeleka hospitalini ili afanyiwe uchunguzi wa kiakili kuthibitisha ikiwa yuko sawa au la,” ikaongezea.
Kulingana na kanuni za polisi, afisa yeyote hafai kuhepa kazi kwa zaidi ya siku 21 bila kufahamisha wakubwa wake mahali aliko.
Wanaofanya hivyo huchukuliwa kuwa wamehepa kazi na wakubwa wao hufika kortini kuomba kibali cha kuwakamata na kuwafunguliwa mashtaka ya kuacha kazi kinyume cha sheria.
Polisi, hata hivyo, hawakutoa sababu kwa nini wameanzisha uchunguzi sasa licha ya Bw Adao kutoweka zaidi ya miezi mitatu iliyopita.