Raila azomewa na wakazi wa Kisumu
RUSHDIE OUDIA Na PETER MBURU
WAKAZI wa Muhoroni katika Kaunti ya Kisumu, Jumatatu walimkemea kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga alipoenda kuzindua mradi wa viwanda eneo hilo.
Wakibeba mabango na kuandamana, wakazi hao walilalamika kuwa serikali inataka kutwaa ardhi yao kwa nguvu ili kujenga mradi huo, wakisisitiza kuwa hawaungi mkono mradi huo, wala hawakushauriwa kabla ya uamuzi huo kufikiwa.
Hatua hiyo ya mapokezi mabaya kwa Bw Odinga ilikuwa ya kushangaza katika ngome yake ya kisiasa, ambako amekuwa akiheshimika kwa miaka mingi na maamuzi yake kupokelewa bila maswali.
Vioja vilianza wakati Bw Odinga aliposema kuwa ujenzi wa mradi huo wa kiuchumi una umuhimu kuliko kuacha ardhi hiyo kuendelea kutumiwa kwa kilimo.
Mara baada ya kutamka hayo, wakazi walimkemea na kupiga makelele, wakisema wanataka kuachiwa ardhi yao badala ya ujenzi wa mradi huo.
“Kwa nini mnaniaibisha? Ninaleta maendeleo ilhali hamuoni miradi ambayo itawafaidi,” Bw Odinga akashangaa.
Vijana hao walichapwa na watu wanaounga mkono ujenzi wa mradi huo na mabango kuharibiwa, huku naye Bw Odinga akijaribu kutuliza hali na kuwarai wakazi kukubali mradi huo.
Alisema mradi huo utajengwa katika ardhi ya ekari 500 na ujenzi utaanza punde tu Sh500 milioni zikitolewa na serikali mwaka huu, huku Sh2.5 bilioni zikitarajiwa kutolewa na serikali mwaka ujao.
“Rais Uhuru Kenyatta, Rais wa Uganda Yoweri Museveni na wa DRC Felix Tshisekedi wanatarajiwa kuzindua rasmi ujenzi wa mradi huo hapo Agosti mwaka huu,” akasema Bw Odinga.
Alikuwa ameandamana na mawaziri Peter Munya wa Biashara na Viwanda, James Macharia wa Uchukuzi na John Munyes wa Madini.
Hata hivyo, ilikuja siku chache tu baada yake na Rais Kenyatta kurejea mikono mitupu kutoka China ambapo walikuwa wameenda kutafuta mkopo wa kuendeleza ujenzi wa Reli Ya Kisasa (SGR) hadi Kisumu, baada ykea kuahidi ujenzi huo.
“Reli mpya ya SGR itajengwa kutoka Naivasha, Narok, Bomet, Sondu hadi Kisumu,” Bw Odinga akaeleza wakazi wa Sondu kabla ya kuandamana na Rais Kenyatta nchini China kuomba mkopo.