Raila, Ruto waachiana majukumu
BENSON MATHEKA NA MWANGI MUIRURI
KIONGOZI wa ODM, Raila Odinga amemuachia Naibu Rais William Ruto majukumu yake ya kinara wa upinzani.
Kwa upande mwingine Dkt Ruto amekabidhi kwa Bw Odinga kazi zake za kutetea Serikali.
Ubadilishanaji huu wa majukumu umeibuka kwa njia isiyo rasmi ukichochewa na mabadiliko ya kisiasa ambayo yamekuwepo nchini tangu 2018.
“Ni wazi kuwa Dkt Ruto na Bw Odinga wamebadilishana majukumu. Dkt Ruto anakosoa serikali huku Bw Odinga akiiunga mkono, tofauti na ilivyokuwa kabla ya handisheki,” asema mdadisi wa siasa Geff Kamwanah.
Bw Kamwanah anatoa mfano wa kauli ya Dkt Ruto ya kushutumu kutumiwa kwa polisi kuwakamata maseneta watatu waliopinga mswada wa ugawi wa pesa za kaunti, na kwa upande mwingine Bw Odinga akawalaumu maseneta wenyewe.
Hii ni kufuatia handisheki ambayo ilizaa ushirikiano kati ya Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta huku Dkt Ruto naye akisukumwa nje na sasa amejipata akitekeleza majukumu ya Kiongozi wa Upinzani.
Naye Bw Odinga amekuwa akipenya ndani ya serikali hatua baada ya hatua hadi akajipoteza makali yake ya kukosoa serikali na kutetea utawala bora na maslahi ya raia. Hii imemgeuza kuwa mmoja wa watetezi sugu wa serikali hata katika maamuzi yenye athari mbaya kwa umma na taifa kwa jumla.
Kabla ya handisheki, Bw Odinga alikuwa mkosoaji mkubwa wa serikali na alichangia katika ufichuzi wa kashfa nyingi za ufisadi na kuhakikisha utawala wa kisheria unazingatiwa na walio madarakani.
Kati ya kashfa alizofichua ni NYS, mabwawa ya Arror na Kimwarer, Eurobond na ununuzi wa kliniki za kuhamishwa, sakata ambazo Dkt Ruto wakati huo alitetea vikali.
Ushirika wake na Rais Kenyatta ulivyoendelea kupata nguvu ndivyo Dkt Ruto alivyojipata kwenye baridi hadi akaamua kuanza kukosoa serikali kwa ufisadi na maamuzi mengine.
Wadadisi wanasema ni kutengwa kwake serikalini kunakomfanya Dkt Ruto kujaza pengo la kiongozi wa upinzani.
“Mambo yanavyoonekana, Ruto amesukumwa kuwa kiongozi wa upinzani 2022,” asema mdadisi wa siasa Javas Bigambo.
Kulingana na Mbunge wa Soy, Bw Caleb Kositany ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Jubilee, hakuna makosa kwa Dkt Ruto na washirika wake kutekeleza majukumu ya upinzani.
“Kwa kuwa sasa ODM wamepatiwa nafasi katika kamati za bunge ambazo zinapaswa kushikiliwa na upande wa walio wengi, tunachoomba ni kuruhusiwa kutekeleza majukumu ya upinzani bungeni ili tuweze kupiga darubini serikali,” Bw Kositany alisema. Mnamo Jumapili, Dkt Ruto alitaja ODM kama “uliokuwa upinzani”, ishara kwamba ameamua kujaza pengo lililoachwa na chama hicho.
Alikuwa akikosoa ODM kwa kutetea sakata ya wizi wa pesa za kukabili janga la corona ambayo inahusishwa na watu wenye ushawishi serikalini.
Hii ilikuwa baada ya Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna, kumkosoa Dkt Ruto kutaka waliohusika kuchukuliwa hatua.
Kauli zake katika Twitter pia zinatoa picha ya mtu asiye serikalini licha ya kuwa ndiye Naibu Rais.
Kulingana na Naibu Mwenyekiti wa Jubilee, David Murathe ambaye ni mwandani mkuu wa Rais Kenyatta, Serikali tayari inamchukulia Dkt Ruto kama mpinzani.
“Rais alipomtaka akomeshe siasa za mapema alikaidi. Anachofanya sasa ni kukemea serikali ambayo yeye ndiye wa pili kwa mamlaka. Hili ni dhihirisho tosha kuwa ameamua kuwa katika upinzani,” Bw Murathe aliambia Taifa Leo.
Mbunge wa Gatanga, Nduati Ngugi naye alisema Dkt Ruto ameonyesha wazi kuwa angependa kupokonywa majukumu yake ya Naibu Rais ili aongoze upinzani.
Hata hivyo, wabunge Ndindi Nyoro wa Kiharu, Kimani Ngunjiri wa Bahati na Alice Wahome (Kandara) pamoja na Rigathi Gachagua (Mathira) wanapuuzilia mbali misimamo hiyo.
Bw Rigathi alisema kuna kundi la wanasiasa wanaotaka kumwangazia Dkt Ruto kama asiye na haki ya kujieleza, hivyo hafai kuzungumza hata wakati mambo yanapoenda vibaya nchini.
Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen na Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi waliambia Taifa Leo kwamba mrengo wa Dkt Ruto hautajibizana na washirika wa handisheki au wa Rais na Jubilee bali wao watazingatia kutetea maslahi ya wananchi.