Rais Kenyatta aagiza timu za uokozi KDF na idara ya polisi zipelekwe Pokot Magharibi
Na CHARLES WASONGA
RAIS Uhuru Kenyatta ameagiza timu za uokozi kutoka kwa wanajeshi wa ulinzi Kenya (KDF) na idara ya polisi kupelekwa katika Kaunti ya Pokot Magharibi iliyokumbwa na maporomoko ya ardhi katika juhudi za kuzuia maafa zaidi.
Kufikia Jumamosi jioni watu zaidi ya 30 walikuwa wamethibitishwa kufariki katika mkasa huo, kulingana na ripoti za Shirika la Msalaba Mwekundu Nchini.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Jumamosi, Rais Kenyatta ametoa hakikisho kuwa serikali yake inafanya kila iwezalo kutoa msaada kwa waathiriwa kwa ushirikiano na mashirika mengine.
“Nimeamuru kwa walinda usalama wetu wapelekwe katika maeneo yaliyoathirika na mkasa wa maporomoko ya ardhi katika Kaunti ya Pokot Magharibi ili kuchukua hatua za kuokoa maisha. Operesheni hiyo itaendelezwa na Wanajeshi wa Ulinzi wa Kenya (KDF), maafisa wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) na wahudumu kutoka Idara ya Mipango Maalum hadi hali ya kawaida itakapoanza kushuhudiwa,” Rais amesema.
Aidha, kiongozi wa nchi amesema amepokea habari za kuhuzunisha kuhusu maporomoko ya ardhi katika Kaunti ya Pokot Magharibi.
Hali hiyo imesababishwa na mvua iliyopitiliza inayoshuhudiwa katika sehemu mbalimbali humu nchini.
“Ninawapa pole waliopoteza wapendwa wao katika mkasa huo na nawatakia waliojeruhiwa na wamepelekwa katika hospitali mbalimbali, afueni ya haraka,” amesema Rais Kenyatta.
Mkasa huo ulitokea mwendo wa nane na nusu alfajiri – yaani usiku wa manane kuamkia Jumamosi – kulingana na Shirika la Msalaba mwekundu na maafisa wa utawala katika maeneo yaliyoathirika. Mojawapo ya maeneo hayo ni kijiji cha Nyarkulian katika kaunti ya ndogo ya Pokot Kusini ambako familia moja ya watu wanane iliangamia walipozikwa hai na matope katika nyumba yao.