Habari

Rais Ruto kutoa Hotuba kuhusu Hali ya Kitaifa Bungeni serikali yake ikipigwa darubini

Na CHARLES WASONGA November 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto ameratibiwa kutoa Hotuba kuhusu Hali ya Kitaifa kwenye kikao maalum cha pamoja cha Bunge la Kitaifa na Seneti Novemba 20, 2025 huku utendakazi wa serikali yake ikipigwa darubini.

Dkt Ruto anatarajiwa kutumia jukwaa hilo, katika ukumbi wa Bunge la Kitaifa, kuangazia mafanikio, changamoto ya serikali yake miaka mitatu baada ya kuapishwa.

Aidha, Rais anatarajiwa kutangaza mikakati inayotekelezwa na serikali ya Kenya Kwanza kuboresha usalama wa kitaifa, kuendeleza umoja na kufanikisha ajenda yake ya maendeleo.

Kulingana na ilani iliyotolewa Jumatano, Novemba 12, 2025 na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula na mwenzake wa Seneti Amason Kingi, kikao hicho kitaanza saa nane na nusu alasiri.

“Kufuatia ilani iliyotolewa na Mheshimiwa William Samoei Ruto, Rais wa Jamhuri ya Kenya na Amiri Jeshi Mkuu la Ulinzi la Kenya, Spika wa Bunge la Kitaifa na Spika wa Seneti wameitisha kikao maalum kitakachofanyika Alhamisi, Novemba 20, 2025 kuanzia saa nane na nusu alasiri kwa ajili ya Hotuba ya Rais.”

“Wabunge na umma wanajulishwa kwamba Kikao hicho Maalum kitafanyika katika Ukumbi wa Bunge la Kitaifa,” notisi  hiyo ikaeleza.

Rais hutoa hotuba ya kila mwaka bungeni, kwa misingi ya Kipengele cha 132 (1) cha Katiba kinamchohitaji kuelezea mipango ya serikali na kutoa utathmini kuhusu utekelezaji wa sera za serikali yake.

Rais pia anahitajika kutoa ripoti kuhusu hatua ambazo serikali yake imepiga katika udhibiti wa usalama wa kitaifa, udumishaji wa maadili ya kitaifa na uzingativu wa majukumu ya kimataifa ya serikali.

Dkt Ruto alitoa Hotuba yake ya mwaka jana Novemba, wakati ambapo joto la kisiasa lilikuwa limetanda nchini kufuatia kuondolewa afisini kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Hotuba ya mwaka huu unajiri wakati ambapo kuna taharuki katika ukanda wa Afrika Mashariki na tathmini ya kina kuhusu utendakazi wa serikali ya Rais Ruto.

Kutekwa nyara na kuzuiliwa kwa raia wa Kenya katika nchi jirani za Uganda na Tanzania pia kumeibua hofu kuhusu ongezeko la visa vya ukiukaji wa haki za kibinadamu katika nchi hizo.