HabariSiasa

Refarenda yaja

June 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

Mabadiliko ya katiba nchini hayawezi kuepukika iwapo Wakenya wanataka kutimiza malengo ya waanzilishi wa taifa hili, Rais Uhuru Kenyatta amesema.

Kwenye hotuba yake ya kuadhimisha Siku Kuu ya 57 ya Madaraka Dei hapo jana, Rais Kenyatta aliwapuuza wanaopinga mageuzi ya katiba akisema ni sehemu ya mambo yanayopaswa kufanywa ili kujenga Kenya mpya.

Hii ilikuwa mara ya kwanza Rais Kenyatta kuzungumzia mjadala unaoendelea wa kubadilisha katiba kupitia mchakato wa Maridhiano (BBI) alionzisha baada ya handisheki yake na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

Ingawa hakumtaja Bw Odinga au BBI kwenye hotuba yake, Rais Kenyatta alinukuu kitabu cha mpiganiaji uhuru marehemu Tom Joseph Mboya, Freedom and After, akisema baadhi ya sehemu za katiba zikikosa kubadilishwa, zinageuka kuwa saratani ya kuangamiza nchi.

“Miaka 55 iliyopita, Mboya alionya Wakenya dhidi ya kukwamilia katiba. Alituambia kwamba katiba yenyewe sio mwisho, ni njia bora ya kuelekea kwenye ufanisi,” alisema Rais Kenyatta.

“Katiba ni stakabadhi iliyo hai. Na ikiwa kuna mambo katika katiba yanayopitwa na umuhimu wake, yanakuwa saratani. Yanafaa kuondolewa au yaambukize mazuri yaliyo katika sheria kuu,” aliongeza.

Aliwakumbusha Wakenya jinsi kifungu cha 2A katika katiba ya zamani kilivyobadilishwa mnamo 1991 baada ya kutumiwa kukandamiza demokrasia ya vyama vingi vya kisiasa nchini, muafaka wa kitaifa ulivyoshirikishwa kwenye katiba kuzima ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2008 na mabadiliko ya katiba ya 2010.

“Miaka 10 baadaye, tayari ninaona ni wakati wa kuibadilisha katiba. Si ya kuondoa katiba ya 2010 lakini kuiimarisha zaidi. Haya ni mabadiliko ambayo yatarekebisha tuliyokosea 2010. Lakini kimsingi, mabadiliko ya kikatiba ninayoazimia ni yatakayokomesha ghasia za baada ya uchaguzi ambazo tumeshuhudia tangu 1992,” alisema.

Kiongozi wa nchi alisema mabadiliko ya katiba anayopigania yatakuza demokrasia na ushirikishi ambao walioandika katiba ya 2010 walinuia.

Akidokeza kwamba mabadiliko hayo yatalenga muundo wa serikali na utawala, Rais Kenyatta alisema, “Hatuwezi kujenga upya taifa letu bila kubadilisha umbo letu la kisiasa. Na muundo huo hauwezi kubadilishwa bila kubadilisha katiba.”

Aidha, alidokeza kuwa mabadiliko hayo yatalenga kifungu cha sita cha katiba kuhusu uongozi na maadili akisema kimeshindwa kudhibiti wanasiasa wafisadi.

“Wakati waandalizi wa kifungu cha sita cha katiba yetu walipokiandika, walitaka kudhibiti tabia. Lakini ni vigumu kudhibiti desturi za kisiasa. Ikiwa tunataka kuwa na Kenya mpya ni lazima tubadilishe tabia yetu iwe ya kuwajibika, kufanya kazi kwa bidii na uadilifu,”alisema. Alisema Kenya inahitaji viongozi waadilifu na sio wanaotumia mamlaka yao kupora mali ili kujitajirisha.

Rais Kenyatta ametangaza vita dhidi ya ufisadi na ni mojawapo ya malengo tisa katika muafaka wake na Bw Odinga. Kwenye hotuba yake, Rais Kenyatta hakusema ni lini katiba itabadilishwa lakini wadadisi wanasema mabadiliko yanayoendelea katika bunge na seneti yanalenga kufanikisha mchakato huo.

Kamati ya watu kumi na wanne aliyoteua kuongoza BBI inatarajiwa kuwasilisha ripoti yake kwake wakati wowote. Kwenye ripoti yake ya awali mwaka jana, kamati hiyo inayosimamiwa na Seneta wa Garissa Yusufu Haji ilipendekeza mabadiliko ya katiba yanayoweza kutekelezwa na bunge na kwenye referenda hasa yanayohusu muundo wa serikali kwa kubuni wadhifa wa waziri mkuu, manaibu wake na yanayohusu ugatuzi.

Wiki jana, Bw Odinga alisisitiza kuwa referenda itakuwa mwaka huu.