HabariHabari za Kitaifa

Rekodi ya maendeleo itampa Ruto Tutam 2027 – Kindiki

Na CECIL ODONGO November 2nd, 2026 Kusoma ni dakika: 2

NAIBU Rais Profesa Kithure Kindiki anatumia mafanikio ya serikali ya Kenya Kwanza katika sekta mbalimbali kuimarisha uungwaji mkono wa Rais William Ruto, huku akiweka msingi wa kusalia katika wadhifa huo kampeni za uchaguzi za 2027 zikichacha.

Katika kipindi cha miaka miwili tangu achukue nafasi ya Rigathi Gachagua, Profesa Kindiki amejitahidi kuonyesha mchango wake katika kuleta udhabiti serikalini akiratibu utekelezaji wa miradi muhimu.

Juhudi zake pia zinaonekana kulenga kuimarisha uungwaji mkono wa Rais Ruto katika ukanda wa Mlima Kenya, ambao ni muhimu katika mipango ya Rais kutafuta muhula wa pili.

Katika tathmini ya utendaji wa serikali, Profesa Kindiki alitetea rekodi ya utawala huo akisema umepiga hatua kubwa licha ya ukosoaji kutoka kwa wapinzani.

“Utawala wa Ruto umefanya vizuri zaidi ya matarajio yaliyowekewa, lakini wakosoaji hawatoi tathmini ya haki kuhusu utendakazi wake. Ukosoaji wao una nia mbaya na hauna ukweli,” akasema.

Alitaja kilimo kama mojawapo ya sekta ambazo serikali imepiga hatua, akisema wakulima milioni 7.9 wa mimea na wafugaji milioni tatu wamesajiliwa ili kurahisisha mipango na utoaji wa huduma.

“Leo tunajua tuna wakulima wangapi, mifugo waliyo nayo, wanakoishi, mazao wanayolima na aina ya mbolea wanayohitaji,” akasema.

Prof Kindiki alisema bei ya gunia la kilo 50 la mbolea imepungua kutoka Sh7,000 mnamo 2022 hadi Sh2,000. Bei ya mbegu bora za mahindi pia imeshuka kutoka Sh300 hadi Sh150 kwa kilo moja.

Aliongeza kuwa wakulima wa kahawa sasa wanapata kati ya Sh130 na Sh150 kwa kilo ya matunda ya kahawa, ikilinganishwa na Sh60 mnamo 2022.

Katika sekta ya afya, alisema Wakenya milioni 33.3 wamejisajili kupata bima ya afya inayofadhiliwa na serikali, ikilinganishwa na milioni nane mnamo 2022.

Kuhusu ajira, alitaja nafasi milioni 1.1 zilizotokana na mpango wa nyumba za gharama nafuu, nafasi 600,000 za ajira nje ya nchi na ajira 350,000 katika sekta ya kidijitali.

“Tumeweza kuwasaidia vijana wengi zaidi kupata ajira na fursa za kujipatia mapato,” akasema.

Pia alitaja kuunganishwa kwa nyumba milioni 1.5 kwenye umeme, kuimarika kwa akiba ya fedha za kigeni na ujenzi wa uwanja wa Talanta wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 60,000.

Profesa Kindiki pia amepata sifa kutoka kwa mawaziri wanaosema amekuwa akiratibu vyema mikutano ya kamati za Baraza la Mawaziri na kuondoa vikwazo vinavyochelewesha miradi.