HabariHabari za Kitaifa

Winnie njiapanda kisiasa uchaguzi wa 2027 ukijongea

Na CECIL ODONGO November 2nd, 2026 Kusoma ni dakika: 2

MBUNGE wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Winnie Odinga, anakabiliwa na utata kuhusu upande wa kisiasa wa kuegemea anapotafuta kiti cha useneta Nairobi katika Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Winnie ameshindwa kuweka wazi iwapo anaunga mkono uongozi wa ODM au vuguvugu la Linda Mwananchi.

Kutokuwepo kwake katika mikutano miwili muhimu Ijumaa na Jumamosi Nairobi kumezidisha maswali kuhusu mwelekeo wake wa kisiasa.

Winnie hakuhudhuria uzinduzi wa makao makuu ya Linda Mwananchi jijini Nairobi wala mkutano wa ODM katika uwanja wa Jacaranda ulioongozwa na viongozi wakuu wa chama hicho.

Katika kuwatambulisha viongozi wa Linda Mwananchi uliofanyika Lavington Ijumaa, kiti cha mbele kilikuwa kimetengewa Winnie, lakini hakufika.

Hali hiyo inatatanisha zaidi kwa sababu Oktoba 15, wakati wa kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kifo cha baba yake Raila Odinga, Winnie alitangaza kuwania useneta Nairobi akisema anataka kufanya hivyo pamoja na vijana.

“Najua watu wengi wamekuwa wakiuliza nilipo na ninakoelekea. Leo nataka kuwajibu ili kuondoa uvumi,” akasema.

“Kwa kuwa Edwin Sifuna anawania wadhifa mwingine, nafasi ya useneta Nairobi iko wazi. Ndiyo maana nimeamua kuwania kiti hicho. Siendi pekee yangu, ninaenda na vijana,” akaongeza.

Matamshi hayo yalifasiriwa kuwa anaegemea Linda Mwananchi, lakini kutohudhuria uzinduzi wake kumezua maswali zaidi.

Hata ndani ya vuguvugu hilo, Winnie anakabiliwa na ushindani kutoka kwa Seneta Maalum, Crystal Asige, ambaye amekuwa akiandamana na Bw Sifuna katika ziara zake za kisiasa.

Pia kuna mvutano kuhusu wagombea wa nyadhifa nyingine Nairobi. Bw Sifuna na viongozi wengine wa Linda Mwananchi wameunga mkono Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino kuwania ugavana, huku aliyekuwa rais wa Chama cha Wanasheria nchini (LSK) Faith Odhiambo akilenga kiti cha mwakilishi wa kike Nairobi.

Profesa Lumala Masibo anasema Winnie anaweza kuwa na nafasi ya kushinda ikiwa atajihusisha na wapigakura na kuzungumza nao badala ya kuonekana kutokuwa na msimamo.

“Ikiwa Winnie atacheza karata zake vizuri ndani ya Linda Mwananchi, anaweza kushinda Nairobi. Lakini ikiwa Babu na Faith watawania, itakuwa vigumu. Winnie, Faith na Babu lazima wakae pamoja na mmoja wao ajiondoe,” akasema.

Katika ODM, Winnie pia anakabiliwa na ushindani kutoka kwa Bw Jalangó ambaye ameungwa mkono na kaka yake Raila Junior kuwania useneta. Raila Junior amesema atabadilisha msimamo wake tu iwapo dada yake atapata tiketi ya chama.

Uhusiano wa Winnie na viongozi wa sasa wa ODM umekuwa na misukosuko tangu kifo cha baba yake. Alipinga kuondolewa kwa Bw Sifuna kama katibu mkuu wa chama Februari mwaka huu.

Katika mkutano wa Kamukunji, eneobunge la Kibra Januari 18, 2026, alikosoa viongozi aliowashutumu kwa kutaka kuchukua usukani wa chama baada ya kifo cha Raila.

“Katika safari hii, sisi tulikuwa abiria na Baba alikuwa dereva. Siku moja tuliamka na kushtuka. Dereva alikuwa amefariki. Baadhi ya watu wakasogea mbele, wakashika usukani na kuuvuta pande tofauti,” alisema.

Winnie pia alizua maswali kuhusu ushirikiano wa ODM na UDA, akisisitiza kuwa maamuzi muhimu yanapaswa kuidhinishwa kwenye Kongamano la Kitaifa la Wajumbe (NDC).

Zaidi ya hayo, alikosolewa na baadhi ya viongozi baada ya kumkashifu Waziri wa Fedha John Mbadi kuhusu namna anavyowahutubia viongozi wa chama akidai alikuwa akiwadharau.

Changamoto zake zimeongezwa na tofauti za kifamilia. Winnie alitawazwa mrithi wa kisiasa wa Raila katika hafla ya Oktoba 4, lakini Raila Junior hakuhudhuria akisema hakujua kuhusu hafla hiyo.

Kwa sasa, Winnie hajapata uungwaji mkono wa wazi kutoka kwa kiongozi mkuu wa ODM wala Linda Mwananchi.

Kutohudhuria mikutano ya hivi karibuni kumeacha maswali kuhusu chama atakachotumia, upande atakaoegemea na uwezo wake wa kuunganisha wafuasi kabla ya uchaguzi wa 2027.