HabariSiasa

Ruto alinidanganya – DCI

March 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

NAIBU Rais William Ruto alisema uwongo kuhusu ziara ya aliyekuwa waziri wa michezo Rashid Echesa ofisini mwake Harambee House Annex mwezi uliopita, Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) ilisema Alhamisi.

Kulingana na picha za CCTV zilizotolewa kwa umma na DCI jana, Bw Echesa na wenzake walikaa katika ofisi ya Dkt Ruto kwa takriban saa moja na dakika 29.

Hii ni kinyume na kauli ya Dkt Ruto wakati sakata hiyo ilipoibuka mwezi uliopita, ambapo alisema kuwa Bw Echesa na wenzake walikaa ofisini mwake kwa dakika 23 pekee.

Bw Echesa alikamatwa muda mfupi baada ya kuondoka ofisini humo na kushtakiwa pamoja na watu wengine wanne kuhusiana na madai ya kupanga kutapeli raia wa kigeni wakidai wangewasaidia kupata zabuni ya kuuzia Kenya vifaa vya kijeshi vya thamani ya Sh39 bilioni.

Mkurugenzi wa DCI George Kinoti alisema mauaji ya mkuu wa usalama katika ofisi ya Dkt Ruto, Sajini Kipyegon Kenei yalihusiana na matukio katika ofisi ya Naibu Rais.

Lakini baadaye jana jioni ofisi ya Dkt Ruto ilikanusha madai ya DCI kuhusu muda ambao Bw Echesa alikaa ofisini humo ikisisitiza alikaa dakika 23.

Kwenye picha za CCTV, Sajini Kenei anaonekana akiwafungulia na kuwaelekeza Bw Echesa na ujumbe wake.

Kwenye taarifa yao kwa DCI, wageni hao walisema walikuwa wameambiwa na Bw Echesa na wenzake kuwa wangeweka sahihi ya kandarasi ya silaha hizo ofisini mwa Dkt Ruto wakati wa ziara hiyo.

Ufichuzi huo kuwa alisema uwongo unatarajiwa kuongeza shinikizo dhidi ya Dkt Ruto, ambaye amejitenga na madai yoyote kuhusu sakata hiyo.

Vile vile, amejitenga na Bw Echesa, akisema kuwa hakuwepo wakati yeye na watu hao walipofika katika afisi yake.

Bw Kinoti aliwaeleza wanahabari kuwa Sajini Kenei alikuwa anatarajiwa kuandikisha taarifa DCI kuhusu ziara hiyo ili kusaidia kutegua kitendawili cha kashfa hiyo ya vifaa vya kijeshi.

“Tulianza uchunguzi kwa njia zetu za kiupelelezi baada ya Kenei kukosa kufika DCI kama alivyotakiwa bila ufafanuzi wowote kutoka kwa maafisa wenzake wala mkuu wao,” akasema Bw Kinoti.

Alieleza kuwa Sajini Kenei aliuawa kinyama, kinyume na ripoti za awali kwamba alijiua.

Bw Kenei alipatikana ameuawa majuma mawili yaliyopita, baada ya kukosekana kwa siku kadhaa wakati DCI walipokuwa wakianzisha uchunguzi kuhusu madai ya utapeli huo wa silaha.

“Marehemu alikuwa amevalia mavazi yake ya kulala na alikuwa amepigwa risasi kutoka chini mwa kidevu chake,” akasema Bw Kinoti.

Kulingana na Bw Kinoti, kilichowashangaza ni kwamba kitanda chake kilikuwa kimetandikwa vizuri, ishara kuwa hakukuwa na dalili zozote za kukabiliana na wale waliohusika kumuua.

Bw Echesa tayari anakabiliwa na kesi mahakamani kuhusu sakata hiyo, ambapo ameshtakiwa kwa ulaghai.

Waziri huyo wa zamani amekuwa akijitetea vikali, akisema kuwa masaibu yanayomwandama ni vita vya kisiasa anazopigwa na mahasimu wake.