Habari

Ruto amzaba Gideon kofi la kwanza la kisiasa

June 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

FLORAH KOECH na WYCLIFF KIPANG

NAIBU Rais, Dkt William Ruto ameanza kuthibitisha kuwa angali anadhibiti eneo la Rift Valley lililo ngome yake ya kisiasa, wakati ambapo wandani wake wanaendelea kuadhibiwa katika Serikali Kuu.

Huku ‘kiboko’ cha Rais Uhuru Kenyatta kikionekana kuelekezwa kwa wandani wa Dkt Ruto katika Bunge la Kitaifa baada ya kumaliza ‘kazi’ katika Seneti, imebainika viongozi wanaoegemea upande wa Naibu Rais nao wameanza kuwachapa mijeledi wandani wa Rais bondeni.

Rais nao wameanza ‘kuwachapa mijeledi’ wandani wa Rais katika eneo la Bonde la Ufa.

Vilevile, imefichuka kuwa Dkt Ruto amekuwa akifanya mikutano ya siri na viongozi na makundi ya wazee wenye ushawishi wa kisiasa katika ukanda huo ili kudhibiti ubabe wake.

Hayo yanajiri wakati ambapo ilifichuka majuzi kwamba shughuli ya kuwaadhibu wafuasi wa kikundi cha Tangatanga itaelekezwa hadi katika taasisi za serikali na yamkini wizara.

Mwandani mkuu wa Seneta wa Baringo, Bw Gideon Moi ndiye sasa aliyejipata pabaya katika siasa za ubabe Bondeni.

Bw Ameja Selemoi ambaye ni mwanchama wa KANU alivuliwa wadhifa wake wa naibu spika katika Bunge la Kaunti ya Baringo.

Hili ni pigo kubwa kwa Seneta Moi ambaye hivi majuzi aliafikiana na Rais Kenyatta kuunganisha vyama vya Jubilee na KANU katika muungano.

Hatua hiyo imeonekana kuinua umaarufu wa Dkt Ruto ambaye amekuwa akitaka kuonyesha ubabe wake kama mfalme wa siasa za Bonde la Ufa huku akijiandaa kuwania urais mwaka wa 2022.

Bw Selemoi, ambaye pia ni Diwani wa Wadi ya Churo/Amaya, alitimuliwa kwa tuhuma za kutumia mamlaka vibaya katika afisi yake.

Alielekea mahakamani kupinga hatua hiyo ya Machi lakini mnamo Ijumaa, Mahakama Kuu mjini Kabarnet iliamua kuwa aliondolewa kwa njia halali.

Nafasi yake sasa imechukuliwa na Diwani wa Wadi ya Kisanana, Bw Jacob Cheboiwo wa Jubilee.

Kulingana na Diwani wa Mochongoi, Bw Kipruto Kimosop, hatua hiyo imethibitisha kuwa kando na tuhuma zinazomkabili Bw Selemoi, Baringo si ngome ya KANU.

“Hili ni onyo kwa wanasiasa wengine wa Chama cha KANU kutoka eneo hili ambao wana tabia ya kumtukana Naibu wa Rais,” akasema Bw Kimosop.

Hatua ya kuunganishwa kwa Kanu na Jubilee hivi majuzi imezidisha uhasama kati ya Dkt Ruto na Seneta Moi ambao wote wanamezea mate kumrithi Rais Kenyatta ifikapo mwaka wa 2022.

Ingawa Seneta Moi anatoka katika Kaunti ya Baringo, Jubilee ndiyo iliyoshinda viti vingi katika uchaguzi mkuu uliopita kikiwemo kiti cha ugavana ambacho kinashikiliwa na Stanley Kiptis.

Dkt Ruto amekuwa akizuru eneo hilo huku mwaka 2019 pekee akitembelea mara 20, zaidi ya ziara amabazo seneta mwenyewe amefanya katika eneo hilo.

Wandani wa karibu wa Seneta Moi kama vile Mbunge wa Tiaty, Bw William Kamket wamekuwa wakiashiria kuwa huenda akagombea urais.

“Kanu itakuwa chama cha kutazamwa mwaka wa 2022,” akasema Bw Kamket.

Alisema chama cha Kanu hivi karibuni kitaanza usajili mpya wa wanachama wake mashinani huku mwaka wa 2022 ukikaribia.

Naibu wa Rais amekuwa akitembelea Kaunti ya Baringo akizindua miradi ya maendeleo ikiwemo mnada maarufu wa mbuzi wa Kimalel ambapo amekuwa akiendeleza siasa zake kwa wenyeji.

Pia suala la eneo ambalo chuo kikuu cha umma cha kwanza kitajengwa limeibua uhasama, ambapo Dkt Ruto anataka kijengwe mjini Kabarnet.

Hadi kifo chake, hayati rais wa zamani Daniel arap Moi alikuwa akipinga kuinuliwa kihadhi kwa chuo cha ufundi cha Baringo ile kiwe chuo kikuu akisema kuwa hatua hiyo itadidimiza vyuo vya kadri.