SAKATA YA NYS: Mawakili wavuna vinono mahakamani
BENSON MATHEKA, VALENTINE OBARA na SAM KIPLAGAT
MAWAKILI zaidi ya 15 wamepata nafasi ya kuvuna vinono kwa kuwakilisha washukiwa wa sakata ya ufisadi katika shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS).
Baadhi ya washukiwa hao 20 waliofikishwa mahakamani Jumanne wameteua mawakili zaidi ya wawili, na wakati huo huo, kuna mawakili ambao wanawakilisha washukiwa zaidi ya wawili kwa wakati mmoja.
Miongoni mwa mawakili waliokuwa mbele ya Hakimu Mkuu Douglas Ogoti katika Mahakama ya Milimani, Nairobi ni Cliff Ombeta, Kirathe Wandungi, Danson Omari, Stanley Kangahi na Stephen Ligunya.
Jumanne, jukumu kuu la mawakili hao lilikuwa ni kujaribu kuthibitishia mahakama kwamba, upande wa mashtaka haukufuata kanuni zifaazo ulipowasilisha kesi zinazohusu ufujaji wa mamilioni ya pesa za umma, na kushawishi korti kuwaachilia huru wateja wao kwa dhamana baada ya kukaa kizuizini tangu walipokamatwa Jumatatu.
Mhadhiri wa sheria Thomas Maosa, alisema kila mshtakiwa huhitaji mwanasheria wa kumshauri kuhusu kesi yake ili haki itendeke.
Kulingana naye, mawakili huwa hawasukumwi na mahitaji ya kifedha kuwakilisha washukiwa wa uhalifu wa aina yoyote bali hitaji la kutekeleza matakwa ya kikatiba.
“Japo uwakili ni kazi, suala hapa sio pesa au kuwa mtu ni mhalifu au mkosaji. Lengo ni kuwakilisha maslahi ya mshtakiwa. Upande wa mashtaka unaweza kutumia ushahidi usio sahihi kuthibitisha kesi. Wakili anaelewa jinsi ya kupima ushahidi na kutambua uongo,” akaeleza.
Sura ya Nne ya Katiba, sehemu ya 50 inasema, kila mshtakiwa ana haki ya kuchukuliwa kama asiye na hatia hadi ithibitishwe vinginevyo, kuwakilishwa na wakili na endapo hawezi kugharamia wakili, serikali inapaswa kumtafutia na kugharamia atakayemwakilisha.
Kwenye mahojiano na Taifa Leo, wakili George Ndichu alisema washukiwa wengi huwa hawana makosa na huishia kuadhibiwa kisheria kwa sababu ya kukosa uwakilishi wa kitaalamu mahakamani.
“Kuna watu ambao hupeleka wenzao kortini kuficha makosa yao na iwapo anayeshtakiwa hana wakili, anaweza kuteseka na hata kufungwa kwa makosa ya watu wengine. Kuna kesi nyingi ambazo hutupiliwa mbali na washtakiwa kuachiliwa huru kwa kukosa ushahidi. Bila wakili, wengi wao wanaweza kuozea jela,” akasema.
Washukiwa waliokuwa mahakamani Jumanne, wakiwemo Katibu wa Wizara ya Utumishi wa Umma, Vijana na Jinsia Lilian Mbogo-Omollo na Mkurugenzi Mkuu wa NYS Richard Ndubai walikanusha mashtaka mbalimbali likiwemo lile utumiaji mbaya wa mamlaka, kupanga njama ya kutenda uhalifu wa kiuchumi na kukosa kufuata kanuni za usimamizi wa fedha za umma.
Hata hivyo, mawakili wengi, akiwemo Bw Ligunya aliyemwakilisha Bi Omollo, walilalamika kuwa upande wa mashtaka ulikuwa unawasilisha mashtaka mengi mapya ghafla na hivyo kuwanyima washtakiwa muda wa kujiandaa kujitetea.
Japo washukiwa ambao hawakuwa kortini walituma mawakili, upande wa mashtaka ulitaka wakamatwe ukisema walikuwa wakifahamu walitakiwa kortini.
Mahakama iliambiwa kwamba hawakuwa na nia ya kufika kortini na walifaa kukamatwa ombi ambalo mawakili wapinga vikali. Miongoni mwa washtakiwa ni wakurugenzi wa kampuni zilizodaiwa kupokea mamilioni ya pesa kutoka kwa NYS bila kutoa huduma au kuuza bidhaa zozote.