VIONGOZI nchini sasa wanajisawiri kama wasiojali wenzao huku wakisalia kukimya Wakenya wanapoumia mataifa ya nje na pia vitisho vinavyotoka kwa majirani zake kuhusu masuala yanayoweza kuvuruga uhusiano mwema wa kidiplomasia.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni ndiye kiongozi wa hivi punde wa ‘kudhalilisha’ Kenya na hata kutishia vita huku serikali nayo ikionekana kutochukulia suala hilo kwa uzito.

Mapema wiki hii, Rais Museveni kwenye mahojiano na redio moja nchini humo alionya kuwa, huenda vita vikazuka siku za usoni iwapo mataifa ya Afrika ambayo hayapakani na bandari yatanyimwa nafasi ya kufikia Pwani.

Hasa alisema Uganda ina haki ya kufikia Bahari Hindi kupitia Kenya akiongeza kuwa kwa miaka kadhaa, Uganda imefungiwa nje ya Bahari Hindi. Hasa, alisisitiza kuwa Kenya inastahili kuacha Uganda ifikie na kutumia bandari jinsi inavyotaka bila kudhibitiwa.

“Hapa Uganda hata ukitaka kujenga bandari, utaijenga kivipi? Hatupakani na bahari nao mfumo wa kisiasa Afrika haujali, “Baadhi ya nchi zetu hazifikii bahari na zimeathirika si kwa sababu za kiuchumi bali kutokana na ulinzi pia.Ukikwama, utasafirisha aje bidhaa zako nje ya nchi?” akauliza Rais Museveni.

“Hii ndiyo maana nina mazungumzo yasiyoisha na Kenya. Hili hukwama na kisha jingine hutokea, mimi mwenyewe pia nina haki ya kutumia bahari kwa sababu ni yangu, hapa mbeleni kutakuwa na vita,” akaongeza.

Mwanawe Museveni ambaye pia ni Kiongozi wa Jeshi Jenerali Muhoozi Kainerugaba alimuunga mkono babake na akaonya kuwa kutakuwa na shida iwapo Kenya ‘itakataa’ kuwaruhusu watumie bandari.

Licha ya onyo hili, serikali ilikimya tu na haikumjibu Museveni moja kwa moja japo matamashi haya yalikuwa ya kichokozi.

Hii ni licha ya kwamba hakujakuwa na tatizo lolote la kidiplomasia kati ya Kenya na Uganda kuhusu uchukuzi wa Bandari ya Mombasa.

Ni baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 ambapo Rais Museveni alilalamika kuwa ghasia ambazo zilifuatia, zilisababisha wafuasi wa upinzani kungóa reli mtaa wa Kibra na kutatiza uchukuzi wa bidhaa hadi Uganda.

Hivi majuzi wanaharakati Bob Njagi na Nicholas Oyoo walizuiwa kwa siku 38 Uganda. Rais Museveni mwenyewe alisema aliwaweka kwenye jokofu kwa siku hizo na kuwaachilia baada ya juhudi za serikali.

Aliwataja kama waliobobea katika kuandaa maandamano na alipata taarifa za kijasusi kwamba walikuwa wandani wa kiongozi wa upinzani Bobi Wine.

Kwa siku hizo, serikali ilikuwa kimya wala haikuwaarifu Wakenya iwapo kulikuwa na juhudi zozote za kuwaachilia Wakenya hao na mahali ambapo walikwepo huko Uganda. Hata kilio cha familia ya Bw Njagi hakikujibiwa na serikali kuhusu alikokuwa mwanao.

Mara si moja, wavuvi kutoka upande wa Kenya wamekuwa wakilalamika kuhangaishwa na polisi wa Uganda katika kisiwa cha Migingo.

Hata hivyo, licha ya ahadi za Rais William Ruto kuwa anashauriana na Rais Museveni kutokomeza utata huo wa miaka mingi, bado hakujakuwa na suluhu huku wavuvi bado wakikumbana na changamoto zile zile za zamani.

Kando na Uganda, Kenya ilikimya tu mmoja wa vinara wa upinzani Martha Karua, aliyekuwa Jaji Mkuu Willy Mutunga na wanaharakati wengine walipofurushwa kutoka Tanzania mnamo Mei 19 mwaka huu.

Viongozi hao walikuwa wakielekea kortini kwenye kesi ambapo Kiongozi wa upinzani Tanzania Tundu Lissu ameshtakiwa kwa uhaini.

Serikali haikuonekana kushujighulisha na suala hilo na hata mwanaharakati Boniface Mwangi alipozuiliwa kisha kutelekezwa mpaka wa Kenya na Tanzania, utawala wa Rais William Ruto haukuonekana kuwatetea raia wake.

Hivi majuzi, Rais wa Tanzania Samia Suluhu alidai wageni waliingilia maandamano nchini humo kupinga ushindi wake.

“Serikali kuendelea kunyamazia shutuma na uchokozi wa mataifa mengine huku Wakenya wakiumia na kudhalilishwa ni jambo ambalo halifai. Kama hivi vitisho vya Museveni, serikali ingemwonya kwa sababu huo ni uchokozi wa wazi ,” akasema Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Martin Andati.