Serikali kutumia machifu shuleni kuhimiza upanzi wa miti
SERIKALI imeanzisha mpango wa kutumia machifu na Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) shuleni katika juhudi zake za kupanda miti bilioni 15 ifikapo mwaka 2032, licha ya kuibuka maswali kuhusu usahihi wa idadi ya miti iliyopandwa hadi sasa.
Rais William Ruto alisema kuwa Kenya imepanda miti bilioni 1.06 katika kipindi cha miaka miwili, lakini ukaguzi wa kina wa takwimu hizo unaibua mashaka.
Kupanda miti hiyo kwa miaka miwili inamaanisha Kenya ilihitaji kupanda zaidi ya miti 1.45 milioni kwa siku, au miti 60,500 kwa saa, sawa na miti 1,010 kila dakika, kiwango kikubwa kinachotia shaka.
kukiwa na watu takriban milioni 50 nchini, kila Mkenya, wakiwemo watoto wachanga na wazee, angetakiwa kupanda angalau mti mmoja kila mwezi kwa miaka miwili ili kufikia idadi hiyo.
Rais Ruto alisema changamoto kubwa imekuwa uhaba wa miche, na kuagiza Wizara husika kuhakikisha Huduma ya Misitu Kenya (KFS) na NYS zinaongeza uzalishaji wa miche ili kufikia miche bilioni mbili.
Alisema mpango wa upanzi wa miti ni wa mashirika mengi, unahusisha jeshi, magereza, sekta ya kibinafsi, Wizara ya Elimu, na wabunge.
“Tunalenga kupanda mti milioni moja leo,” alisema Ruto, akieleza kuwa upanzi wa miti pia ni sehemu ya kuhakikisha utoshelevu wa chakula na kuimarisha mazingira kwa kuongeza mvua na kuhifadhi maji.
Waziri wa Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi na Misitu, Deborah Barasa, alisema serikali sasa inalenga zaidi miti ya matunda, hasa shuleni, ikidaiwa kuwa miti milioni 500 ya matunda ilipandwa mwezi Oktoba pekee.
Hata hivyo, changamoto kubwa ni kufuata na kuthibitisha idadi halisi ya miti iliyopandwa na kudumu kwake. Kwa sasa, serikali inatumia machifu na maafisa wa serikali kutoa ripoti kuhusu miti iliyopandwa katika maeneo yao.
Susan Boit, mratibu wa kitaifa wa Mpango wa Kupanda Miti Bilioni 15, alisema wamezindua app ya kidijitali iitwayo Jaza Miti, ambayo itasaidia kufuatilia idadi halisi ya miti.
Amehimiza mashirika ya kibinafsi na wahisani kutoa taarifa za uendelevu wa upand miti, huku serikali ikipanga kupanda miti katika maeneo yaliyokatwa, maeneo ya mijini, maeneo kame, na misitu ya kibinafsi na ya kibiashara.
Mpango huu mkubwa wa mazingira unatarajiwa kusaidia Kenya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, uhaba wa maji, na matatizo ya uzalishaji chakula kwa njia endelevu.