Habari

Serikali yajiandaa kukopa mabilioni tena

October 31st, 2018 Kusoma ni dakika: 3

Na VALENTINE OBARA

WAKENYA wataendelea kukabiliwa na ugumu wa kimaisha kwa kipindi kirefu zaidi kutokana na uwezekano wa ushuru na gharama ya maisha kuongezeka tena. Hii ni baada ya kufichuka kwamba Serikali inapanga kuchukua mkopo mpya wa Sh287 bilioni.

Uhaba wa fedha kwenye hazina ya taifa katika bajeti ya mwaka huu ya Sh3 trilioni ulipelekea serikali kuongeza ushuru wa bidhaa mbalimbali ikiwemo mafuta, huduma za mawasiliano ya simu na huduma za kifedha, na ukopaji huu mpya utalazimu serikali kuongeza ushuru zaidi kulipa madeni yanayoongezeka.

Habari hizi zimechipuka wiki chache tu baada ya Serikali kurundikia mwananchi ushuru kwa bidhaa za kimsingi kama vile petroli, dawa za kilimo, Mpesa na kupiga simu. Pia ushuru wa kugharamia nyumba zitakazojengwa na serikali unatarajiwa kuanza karibuni.

Katibu wa Wizara ya Fedha, Dkt Kamau Thugge, alinukuliwa akisema serikali itakopa Sh250 bilioni za Eurobond na Sh37 bilioni kutoka kwa mashirika ya kifedha ili kujaza pengo la mahitaji ya kifedha kwenye bajeti ya mwaka huu.

Ripoti hizo zilizochapishwa na mtandao wa habari za uchumi wa Bloomberg mnamo Jumatatu, zimewadia wakati ambapo madeni ya Kenya yamefika zaidi ya Sh5 trilioni tangu wakati Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto walipoingia mamlakani, na imebashiriwa yatafika Sh7 trilioni watakapomaliza kipindi chao cha utawala 2022.

Ukopaji huo wa Eurobond ni wa tatu kwa serikali ya Jubilee baada ya ule wa Sh200 bilioni mnamo Februari mwaka jana na Sh275 bilioni mnamo 2014.

Kulingana na Shirika la Fedha Duniani, deni la Kenya litafikia asilimia 63.2 ya utajiri wa nchi mwishoni mwa mwaka huu, hali ambayo inaweka uchumi katika hatari ya kuyumba na pia shilingi ya Kenya kupoteza thamani.

Wiki iliyopita, IMF ilishauri serikali ichukue hatua za kupunguza madeni yake ambayo yanazidi kuongezeka, na hivyo hatua ya kutangaza mkopo wa kukopa madeni mapya inatilia shaka kujitolea kulinda mwananchi kutokana na gharama kubwa ya maisha.

Bloomberg inamnukuu mwanauchumi wa benki ya CBA, Faith Atiti akisema mpango huu mpya wa kukopa Eurobond unaweka kwenye hatari kubwa: “Uuzaji wa Eurobond mpya wakati ambapo kuna deni kubwa na riba za juu kimataifa kutaathiri zaidi shilingi,” alieleza Bi Atiti.

Kiasi kikubwa cha fedha za umma kinatumiwa kulipa madeni mbali na kugharamia mahitaji mengine ya kuendesha serikali ingawa kumekuwepo sakata za ufisadi ambapo mabilioni ya fedha za umma zilifujwa.

Rais alipohojiwa Jumatatu na kituo cha CNN kuhusu madeni mengi yaliyochukuliwa na serikali yake, alisema hana wasiwasi kuyahusu kwa vile anaamini fedha anazokopa hutumiwa kustawisha maendeleo ya nchi.

“Ningekuwa na wasiwasi kama fedha tunazokopa zingekuwa zinatumiwa kwa mahitaji ya kawaida kama vile kulipa mishahara. Lakini mikopo tunayochukua hutumiwa kuimarisha miundomsingi,” Rais aliambia CNN.

Kulingana na Rais, lengo la awamu ya kwanza ya uongozi wake lilikuwa ni kuboresha miundomsingi kama vile barabara, reli ya kisasa na usambazaji wa stima ili kutoa mazingara bora kwa wawekezaji kufanya biashara, na hivyo kuongeza nafasi za ajira kwa wananchi.

Katika awamu ya pili, Rais alisema analenga kutimiza miradi itakayoboresha maisha ya wananchi moja kwa moja kama vile huduma za afya na makao bora kwa bei nafuu.

Lakini wataalamu wa kiuchumi wanaonya kuwa taifa linafaa kujihadhari na madeni makubwa kwani kuna uwezekano nchi ishindwe kulipa baadaye.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa na uongozi, Bw Morris Odhiambo anasema haina maana serikali kukopa madeni mengi ikidai ni ya kuleta maendeleo kwa manufaa ya wananchi ilhali wananchi wanazidi kuteseka kutokana na ushuru mkubwa.

“Hivi sasa tayari tunashuhudia athari za mikopo iliyochukuliwa awali. Haya madeni yataleta athari kwa uchumi kwa muda mrefu. Unapotoza wananchi ushuru mkubwa, hawataweza kutumia fedha kwa mahitaji mengine na matokeo yake ni kwamba uchumi utakuwa hafifu,” akasema.

Kulingana naye, ni kinaya serikali kudai inalenga kuwezesha wananchi kuishi vyema kwa gharama nafuu ajenda nne kuu, ilhali wananchi hao hao ndio wanaotozwa ushuru mkubwa kupita kiasi kugharamia miradi hii.

“Kile ambacho serikali inastahili kufanya ni kuweka mazingara bora ili mwananchi awe na uwezo wa kujikimu kifedha ili aweze kugharamia mahitaji kama vile nyumba, chakula na afya bora. Vinginevyo wananchi hawatafurahia matunda ya miradi hii,” akaeleza.