Shangwe kijijini mwanafunzi kuongoza #KCPE2019 kwa alama 440
Na REGINA KINOGU
VIFIJO na shangwe zimeshuhudiwa Jumatatu katika kijiji cha Maragima, eneobunge la Kieni, Kaunti ya Nyeri baada ya Andie Munyiri kutangazwa mwanafunzi bora kitaifa kwenye mtihani wa mwaka huu wa darasa la nane (KCPE) kwa kuzoa alama 440.
Munyiri, ambaye alisomea katika shule ya Damacrest Academy iliyoko mtaa wa Uthiru, Kaunti ya Kiambu, alipata habari hizo akiwa Kaunti ya Nyeri alikokuwa ameenda kuwatembelea nyanya na babu yake.
Aliambia Taifa Leo kuwa alipata motisha wa kutia bidii masomoni baada ya babake kumwahidi angemnunulia laptopu na kumpeleka safari katika mkahawa wa The Ark ulioko Nyeri iwapo angepata alama 420 kwenda juu..
‘Ahadi ya baba ilinitia motisha wa kusoma kwa bidii zaidi,’ akasema mvulana huyo aliyekuwa amechangamka.
Alisema alitarajia kupata matokeo bora lakini hakuwa akidhani angeweza kuwa mwanafunzi bora wa KCPE wa mwaka wa 2019.
Alieleza kuwa matumaini yake ni kujiunga na shule ya Alliance Boys kisha chuo kikuu kusomea uhadisi ili awe kama babu yake.