Habari

Sheria yasukwa kupandisha umri wa kunywa pombe hadi 21

Na STEVE OTIENO July 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KENYA inapanga kuongeza umri wa mtu kuruhusiwa kunywa pombe kutoka miaka 18 hadi 21 ili kudhibiti uraibu wa pombe, hasa miongoni mwa vijana.

Aidha, serikali inapania kupiga marufuku uuzaji wa pombe mitandaoni, uwasilishaji wa pombe manyumba na uuzaji wa vileo hivyo karibu na shule na makanisa.

Kanuni hii mpya ni sehemu ya mapendekezo yaliyoko katika sera mpya ya Kitaifa kuhusu Matumizi Mabaya ya Pombe na Mihadarati ya 2025. Sera hiyo inalenga kudhibiti changamoto ya uraibu wa pombe na mihadarati ambayo imevuruga familia kadhaa na kupunguza kasi ya maendeleo kitaifa.

Baraza la Mawaziri, kupitia taarifa iliyotolewa Juni 24, imeiagiza Mamlaka ya Kitaifa ya Kupambana na Matumizi mabaya ya Pombe na Mihadarati (Nacada) itekeleza mabadiliko yalipendekezwa katika sera hii mpya.

Nacada itashirikiana na serikali za kaunti katika kufanikisha utekelezaji wa kanuni hizo mpya. Aidha, itapata usaidizi kutoka kwa asasi za usalama na viongozi wa kijamii kote nchini.

Kulingana na takwimu za hivi punde kutoka kwa Nacada, karibu asilimia 13 ya Wakenya wenye umri kati ya miaka 15 na 65 (karibu watu milioni 4.7 ) hunywa pombe.

Idadi kubwa wa waraibu wa vileo hivyo ni vijana wenye umri wa kati ya miaka 18 na 24.

Ajabu ni kwamba karibu mwanafunzi mmoja kati ya 10 wanaosomea shule za upili walikubali kwa wamewahi kutumia pombe huku umri wa wanaotumia vileo kwa mara ya kwanza ukipungua kila mwaka.

Isitoshe, watoto wenye umri wa mwaka mdogo wa kati ya miaka sita na tisa pia wanashawishiwa kunywa pombe manyumbani mwao na majirani.

Kero la unywaji pombe na madhara yake ni wazi kote nchini; kuanzia mijini hadi mashambani.

Pombe inauzwa karibu na shule, makanisa na hata makazi. Aina mbalimbali za mvinyo wa bei rahisi inaendelea kuuzwa zikiwa zimepakiwa kwenye chupa na karatasi za plastiki.

Vijana wengi hunywa pombe ili kujisahaulisha na changamoto za ukosefu wa ajira, kuvunjika kwa familia zao, ushawishi kutoka kwa wenzao au kwa sababu pombe zinapatikana kwa urahisi kwa bei nafuu.

Kupandishwa kwa umri wa mtu kuruhusiwa kunywa pombe hadi miaka 21 kunaiweka Kenya katika nafasi sawa na nchi kama Amerika, ambako utafiti umeonyesha kuwa hatua hiyo inapunguza uraibu wa pombe miongoni mwa vijana.

Ni sehemu ya mpango mpana wa kuwazuia tatizo la vijana kukolea unywaji pombe, ongezeko la visa vya wanafunzi kufanya vibaya katika mitihani, ongezeko la visa vya dhuluma ya kijinsia na kudhoofika kwa afya ya kiakili.

Chini ya kanuni hizi mpya, itakuwa mafuruku kwa mfanyabiashara kuuza pombe ndani ya umbali wa mita 300 kutoka taasisi za masomo, maeneo ya kuabudu na mitaa ya makazi.

Hatua hii italazimisha baa nyingi kuhamishwa kwingineko au kufungwa kabisa.