Habari

SIASA: 'Minji minji' wahisi joto

June 14th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na WANDERI KAMAU

BAADHI ya wanawake wanasiasa waliosisimua wapigakura na kuchaguliwa kwa kishindo mnamo 2017, wamejipata wakikabili mawimbi makali ya siasa yanayotishia kuzamisha ndoto zao.

Kuchaguliwa kwao kulivumishwa na upepo wa msimbo wa “Minji Minji”, ambapo wapigakura waliwaona kama kizazi kipya cha viongozi wanawake ambao wangeleta mwamko mpya wa siasa nchini.

Kimaumbile, wameumbwa wakaumbika, ni wenye mvuto kwa sura, wameelimika, wakakamavu, wana ufasaha mkubwa wa lugha ya wanasiasa na weledi wa kusisimua kwa miondoko yao jukwaani.

Mbali na sifa zingine zilizowafaa, urembo wao pia ulisisimua baadhi ya wapiga kura walioshawishika kuwachagua.

Hata hivyo, wengi wao sasa ndani ya bahari iliyochafuka na inayotisha kuwazamisha baadhi kisiasa.

Wanasiasa hao “minji minji” ni pamoja na Gavana Anne Waiguru (Kirinyaga), Seneta Susan Kihika (Nakuru), Seneta Maalum Millicent Omanga (Jubilee), Bi Catherine Waruguru (Mwakilishi wa Wanawake (Laikipia), Aisha Jumwa (Mbunge wa Malindi) na Bi Cecily Mbarire (Mbunge Maalum).

Upeo wa masaibu yao ulidhihirika mnamo Jumanne wiki hii, baada ya madiwani katika Bunge la Kaunti ya Kirinyaga kupitisha hoja ya kumng’oa mamlakani Bi Waiguru kwa tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya ofisi.

Gavana Waiguru alipata pigo mnamo Alhamisi wakati Mahakama Kuu jijini Nairobi ilipotupilia mbali ombi la kuitaka kufutilia hoja ya kuondolewa kwake.

Macho yake sasa yamo kwenye Seneti ambayo inatarajiwa kutathmini na kujadili hoja ya kumtimua siku ya Jumanne.

Bi Kihika naye alichaguliwa kwa kishindo kuwa Seneta wa Nakuru, baada ya kuonyesha ukakamavu mkubwa alipohudumu kama Spika wa Bunge la Kaunti hiyo kati ya 2013 na 2017.

Nyota yake kisiasa iling’aa zaidi alipochaguliwa na Chama cha Jubilee kuwa Kiranja wa Wengi kwenye Seneti, baadhi ya wadadisi wa siasa wakisema rekodi yake nzuri kama Spika wa Nakuru ndiyo ilichangia wengi kuwa na imani naye.

Hata hivyo, giza lilionekana kumwangukia mwezi uliopita alipong’atuliwa kutoka nafasi hiyo kwa madai ya kukiuka “kanuni na masharti” ya Jubilee.

Bi Kihika amekuwa miongoni mwa wanasiasa wa kundi la ‘Tangatanga’ ambalo limekuwa likimuunga mkono Naibu Rais William Ruto kuwania urais 2022.

Wembe huo huo ndio ulimnyoa Bi Mbarire, ambaye alivuliwa wadhifa wake kama Naibu Kiranja wa Wengi katika Bunge la Kitaifa.

Bi Omanga naye aliteuliwa Seneta Maalum na Jubilee, baada ya kushindwa kupata tiketi ya kuwania nafasi ya Mwakilishi wa Wanawake katika Kaunti ya Nairobi mnamo 2017.

Kwa sasa Bi Omanga, maarufu kama “Mama Miradi” ni miongoni mwa maseneta watano maalum ambao wanakabiliwa na kamati ya nidhamu ya Jubilee, kwa madai ya kukiuka kanuni zake.

Yeye pia ni miongoni mwa viongozi ambao wamekuwa wakimfanyia kampeni Dkt Ruto.

Na katika kile kilionekana kama njia ya “kukwepa” adhabu ya chama, Bi Waruguru ameingiza baridi na kuhama katika kambi ya Dkt Ruto.

Baada ya kukutana na Kinara wa ODM Raila Odinga mapema wiki hii, Bi Waruguru alisema kuwa anaunga mkono handisheki kati ya kinara huyo na Rais Uhuru Kenyatta.

Kambi ya Dkt Ruto imekuwa vuguvugu kuhusu handisheki na hatua yake kubadili kauli ni ishara kuwa ameyeyuka katika msimamo wake wa awali.

Bi Jumwa naye alijipata matatani baada ya kuondolewa kama mwanachama wa Kamati ya Huduma za Bunge (PSC) na ODM kwa madai ya kukiuka kanuni za chama.

Mbunge huyo ni miongoni mwa viongozi wa Pwani ambao wamekuwa nyuma ya Dkt Ruto, akionekata kutotishika hata kidogo licha ya hatua za kinidhamu ambazo amekuwa akichukuliwa na ODM.

Wabunge hao “minji minji” wanasema kuwa masaibu wanayopitia kwa sasa ni kuonewa na kuendelezwa kwa unyanyasaji wa wanawake.

“Sitaki kukosoa uamuzi wa chama kuniondoa kwenye nafasi yangu kwani kina haki kufanya maamuzi yake. Hata hivyo, lazima mchakato na taratibu zifaazo zifuatwe, na katika kuondolewa kwangu hayo hayakuzingatiwa,” asema Bi Kihika.

Seneta huyo pia analaumu migawanyiko ya wanawake kama kikwazo kikuu kwa wengi wao kukosa kung’aa kwenye ulingo wa siasa.

Bi Jumwa naye anakosoa vyama vya kisiasa kama taasisi ambazo zimekosa imani na wanawake, akisema vingi haviwapi uhuru wa kujieleza.

“Mimi nimeadhibiwa kwa kueleza msimamo wangu kisiasa. Hilo si kosa bali ni haki yangu kwani tuko katika nchi inayozingatia demokrasia,” akasema.

Hata hivyo, Bw Javas Bigambo ambaye ni mchanganuzi wa siasa anasema kuwa ingawa Katiba imepanua nafasi kuhusu uongozi wa wanawake, wengi wao hawajadhihirisha uwezo wao.

“Bado tuna safari ndefu kuhakikisha tuna wanawake waliomakinika katika siasa,” asema.

Baadhi ya viongozi anaowataja kuwa mfano wa kuigwa ni magavana Charity Ngilu (Kitui) na marehemu Dkt Joyce Laboso (aliyekuwa gavana wa Bomet).