HabariSiasa

Sijawahi kuiba hata ndururu ya mtu – Ruto

July 10th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

NAIBU Rais William Ruto ameapa kuwa hajawahi kuiba hata ndururu ya mtu maishani mwake, kinyume na uvumi ambao umekuwa ukimhusisha na uporaji wa mali ya umma.

“Nataka kusema mbele ya Wakenya bila kusita kuwa sijawahi kuiba hata ndururu ya mtu,” alisema Bw Ruto wakati wa mahojiano ya moja kwa moja na runinga ya NTV mnamo Jumapili jioni.

Alisema yuko tayari kufanyiwa ukaguzi wa jinsi alivyojipatia mali yake akisema amechangamkia hatua hiyo ili kunyamazisha wale ambao wamekuwa wakimhusisha na wizi wa mali ya umma.

“Wakati huo ukifika nitaweka wazi nilivyopata kila ninachomiliki. Hili litakuwa wazi na kila mmoja atajua niliyo nayo,” akasema.

Kumekuwa na uvumi katika midahalo ya kijamii na pia mitandao kuwa Naibu Rais amejilimbikizia mali nyingi inayodaiwa imetokana na ufisadi.

Lakini mnamo Jumapili, Bw Ruto alisema imekuwa kawaida kwa Wakenya kuwaona watu waliotoka familia maskini wanapotajirika kuwa wameiba.

“Mtoto wa maskini anapotajirika inasemekana ni mali ya wizi. Mtoto wa tajiri akitajirika hiyo ni mali ya babake. Huu ni mtazamo uliojaa ubaguzi,” akaeleza.

Kufuatia mahojiano hayo, vyama vya Jubilee na ODM vilichongoana mtandaoni kila kimoja kikidai kuwa na wafuasi wengi na maarufu nchini.

Jubilee kilijigamba kuwa ndicho chama kikubwa nchini Kenya na kitampatia Bw Ruto tiketi ya kugombea urais.

Kwenye ujumbe kupitia Twitter, chama hicho kilisema kimeungana, ndicho kikubwa zaidi nchini na kwamba kina mgombea urais mmoja kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 ambaye ni Bw Ruto.

“Tumeungana, JP ndicho chama kikubwa zaidi katika Jamhuri na mgombea urais wetu 2022 ni William Ruto licha ya juhudi za NTV kumhangaisha kwenye mahojiano ya moja kwa moja kwenye runinga,” Jubilee kilisema.

Pia kilielezea kutoridhishwa na jinsi mtangazaji wa NTV Mark Maasai alivyomsukuma Naibu Rais kujibu maswali.

Dakika chache baada ya ujumbe wa Jubilee, ODM kiliandika kwenye Twitter: “Jubilee kinawezaje kujiita chama kikubwa wakati ambapo hakina mfumo na ofisi za matawi isipokuwa ofisi ya kitaifa? Kinalipa wafanyakazi kama vibarua, ni aibu kujiita chama cha kisiasa,” ODM kilisema.

Ni jumbe ambazo hazikutarajiwa ikizingatiwa kuwa Rais Uhuru Kenyatta ambaye ni kiongozi wa Jubilee na Raila Odinga ambaye ni kiongozi wa ODM walikubali kushirikiana baada ya kusalimiana Machi 9 mwaka huu.

Viongozi hao waliamua kuzika tofauti zao na kuunganisha Wakenya.

Hata hivyo, wabunge wa ODM wamekuwa wakimlaumu Bw Ruto kwa kutokumbatia muafaka huo kikamilifu japo amesisitiza kuwa anaunga juhudi za kuunganisha Wakenya.

Kwenye mahojiano hayo, Bw Ruto alisema japo hakushirikishwa kwenye mazungumzo yaliyotangulia muafaka huo, Rais Kenyatta alimfahamisha na akakubali.

Huku Jubilee kikidai kimeungana baadhi ya wabunge kutoka eneo la Mlima Kenya ambalo ni ngome ya Rais Kenyatta wamepinga uwezekano wa kumuunga Bw Ruto kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Wiki mbili zilizopita baadhi ya wazee wa jamii ya Agikuyu walimtaka Ruto kustaafu siasa pamoja na Rais Kenyatta 2022 jambo ambalo wadadisi wanasema mpasuko katika Jubilee. Ruto alijitokeza na kusema hana deni la kisiasa na mtu au jamii yeyote.