Sishuki hapa bila chai, mahabusu awahangaisha askari
Na GERALD BWISA
KULIZUKA kizaazaa katika mahakama ya Kitale Jumanne asubuhi baada ya mmoja wa mahabusu kukataa kushuka kutoka kwa lori la gereza ili ahudhurie kikao cha kesi yake, akitaka kwanza apewe chai.
Mambo yalikuwa shwari lori hilo lililokuwa limejaa mahabusu wengine lilipoegeshwa katika uga wa mahakama, na kila mmoja akaanza kushuka kuingia kortini.
Hata hivyo, ilipowadia zamu ya mfungwa huyo aliye rumande, aliyetambulika tu kama Stephen, alipanda juu ya lori na kuanza kupiga kelele akitaka apewe chai kwanza.
“Mimi sitoki hapa hadi nipewe chai,” akasema kwa nguvu.
Askari wa magereza waliosafiri na mahabusu hao ili kutoa ulinzi walipigwa na butwaa kabla kujikusanya na kuafikiana kumtuma mmoja wao akamshushe chini mtu huyo kwa lazima.
Maji yalizidi unga pale Stephen alimpiga chenga akiruka kutoka upande mmoja hadi mwingine kumkwepa askari huyo.
Lakini ujanja wake ulifika kikomo aliponaswa na kuteremshwa chini.
Aidha, hakupewa hata tone ya chai huku akisindikizwa haraka upesi hadi seli na kupewa onyo kali akithubutu kurudia tena utundu huo.
Stephen anakabiliwa na shtaka la kuiba mahindi eneo la Cherangany. Alikuwa amefikishwa kortini pamoja na washtakiwa wengine ili kusikizwa kwa kesi hiyo.