Sitakubali tena kuwa mgombea mwenza – Kalonzo
Na KITAVI MUTUA
KIONGOZI wa Wiper Jumatatu alitangaza hatakubali tena kuwa mgombea mwenza kwenye uchaguzi wa urais na kusisitiza atagombea kuongoza taifa 2022.
“Wakamba wameerevuka zaidi kutokana na chaguzi tatu zilizopita. Wakati wa kucheza nafasi ya pili umepita. Lakini tutashirikiana na jamii zingine katika uchaguzi wa 2022,” alisema Bw Musyoka.
Msimamo wake uliungwa mkono na Gavana wa Kitui, Charity Ngilu ambaye pia alitangaza kuwa atajiunga rasmi na chama cha Wiper na kuahidi kuwa ataongoza kampeni za Kalonzo Musyoka kuwania uraia 2022.
Bi Ngilu alisema licha ya kuwa mpinzani mkubwa wa Bw Musyoka kwa muda mrefu, hayo sasa ni historia.
“Nitaongoza juhudi za kuhakikisha kwamba Bw Musyoka anapata fedha za kutosha za kumwezesha kufanya kampeni 2022,” akasema Bi Ngilu.
Mkutano huo uliitishwa katika jaribio la kuunganisha jamii ya Wakamba.
Gavana wa Machakos Alfred Mutua hakufika kwenye kikao hicho kilichoandaliwa Komarock Ranch katika Kaunti ya Machakos akisema ulikuwa mkutano wa Wiper.
“Tunaunga mkono juhudi za kutaka kuunganisha jamii ya Wakamba ili kujadili masuala ya kiuchumi yanayoweza kunufaisha watu wetu.
Lakini chama cha Chap Chap hakiko tayari kuhudhuria kikao ambacho lengo lake ni kuinua mtu fulani ili kupata nafasi ya kujitafutia nyadhifa,” akasema Dkt Mutua.
Kauli ya Muthama
Akihutubia mkutano huo, aliyekuwa Seneta wa Machakos, Bw Johnstone Muthama alimshambulia kiongozi wa ODM Raila Odinga kwa kuwatenga vinara wenzake wa muungano wa NASA kwenye mwafaka wa maelewano na Rais Uhuru Kenyatta.
Bw Muthama alimtetea Bw Musyoka na vinara wenzake wa NASA Musalia Mudavadi (ANC) na Seneta Moses Wetang’ula (Ford-Kenya) kwa kuhepa hafla ya kuapisha Bw Odinga uwanjani Uhuru Park mnamo Januari 30.
“Nilikuwa katika kamati ya kuandaa hafla ya kumwapisha Bw Odinga lakini siku hiyo ilipowadia nilikataa kuhudhuria kwa sababu nilijua kwamba shughuli hiyo ilikuwa bure, sawa na kufukuza upepo,” akasema Bw Muthama.
Gavana Kivutha Kibwana wa Makueni alisema mkutano wa Jumatatu ulikuwa wa kuleta jamii ya Wakamba pamoja na wala haulengi kumdunisha kiongozi yeyote ambaye hakuhudhuria.
“Viongozi ambao hawakujitokeza katika mkutano huu si maadui bali tunafahamu kuwa wao pia wanataka jamii yetu kuungana,” akasema Prof Kibwana.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wanasiasa, viongozi wa kidini, wasomi na wakazi wa kaunti za Machakos, Kitui na Makueni.