Siwezi kujaza fomu za uraia, afoka Miguna Miguna
Na STELLA CHERONO na BENSON MATHEKA
WAKILI mbishi Dkt Miguna Miguna anaendelea kuzuiliwa katika uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) Nairobi huku wakili wake Cliff Ombeta akisema hatajaza fomu alizopatiwa na idara ya uhamiaji.
Bw Ombetta alisema Jumanne kwamba mteja wake hataomba upya uraia wa Kenya kwa sababu kufanya hivyo ni sawa na Miguna kukubaliana na serikali kwamba hakuwa raia wa Kenya.
Aliitaka serikali kuheshimu agizo la Mahakama Kuu ambalo iliagiza Miguna kurudi Kenya baada ya kupelekwa Canada kinyume cha sheria.
“Anapaswa kuruhusiwa kuingia Kenya kwa nguvu za agizo la mahakama,” Bw Ombetta aliambia wanahabari katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA).
Alisema kujaza fomu alivyotakiwa na idara ya uhamiaji ni kumaanisha kwamba Miguna anakubali kwamba serikali ilikuwa sawa tangu mwanzo kwamba alikuwa nchini kinyume cha sheria.
“Serikali inataka atumie paspoti yake ya Canada kuthibitisha vitendo vyake, wanataka apatiwe viza ili iweze kumpimia muda atakaokuwa Kenya,” alisema.
Alisema kwamba Mahakama Kuu iliagiza serikali ihakikishe wakili huyo amerudi Kenya na kumpatia paspoti na sio kuomba mpya.
“Mahakama ilisema anafaa kuwa nchini hadi kesi yake imalizike. Hatujui itachukua muda gani. Mahakama iliagiza aruhusiwe kuingia Kenya bila masharti,” alisema Bw Ombetta.
Bw Ombetta ambaye aliandamana na katibu mkuu wa ODM Edwin Sifuna, hakuruhusiwa kuingia eneo ambalo Miguna amefungiwa katika chumba kimoja. Alisema haruhusiwi kuona yeyote.
Kufikia adhuhuri Jumanne, mawakili James Orengo na Otiende Amollo walikuwa katika eneo la kusubiri wageni wakitarajia kumuona na kuzungumza na Bw Miguna.
Maafisa wa kikosi cha kupambana na fujo (GSU) waliwafukuza mawakili na wanahabari na kuzingira eneo ambalo Miguna amezuiwa.