HabariSiasa

Sonko agawanya ODM

February 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

VIONGOZI wa Chama cha ODM sasa wamegawanyika kuhusu ikiwa madiwani wanastahili kumng’oa mamlakani Gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko.

Baadhi ya madiwani katika Bunge la Kaunti ya Nairobi wamekuwa wakisema kuna mipango ya kumfurusha Bw Sonko ambaye alikatazwa na mahakama kuingia afisini mwake hadi wakati kesi yake kuhusu ufisadi itakapokamilika.

Katika Chama cha ODM, baadhi ya madiwani huwa wako katika mstari wa mbele kuunga mkono juhudi za kumtimua gavana huyo, lakini kuna wengine wanaopinga.

Jana, Mwenyekiti wa chama hicho katika Kaunti ya Nairobi, Bw George Aladwa, na Katibu Mkuu wa chama, Bw Edwin Sifuna walitoa taarifa za kutofautiana kuhusu msimamo wa chama.

Kwa mujibu wa barua iliyoandikwa na Bw Aladwa, Kiongozi wa Chama, Bw Raila Odinga alikuwa ameagiza wanachama wasiunge mkono shughuli zozote za kumwondoa Bw Sonko mamlakani.

“Kumekuwa na madai yanayoenea kwamba chama chetu kinaunga mkono kufurushwa kwa Gavana Mike Mbuvi Sonko. Nimeagizwa na kiongozi wa chama, Bw Raila Odinga kushauri madiwani kuwa chama hakiungi mkono hatua hiyo,” akasema.

Bw Aladwa alionya madiwani dhidi ya kutia sahihi kwa pendekezo lolote la kumtimua Bw Sonko isipokuwa kama chama kitaagiza hivyo.

Hata hivyo, Bw Sifuna ambaye ndiye msemaji wa chama alipuuzilia mbali barua hiyo na kusema mawasiliano rasmi kutoka kwa ODM yanafaa kutoka kwake kama Katibu Mkuu, wala si kutoka kwa afisa mwingine yeyote hasa wanaosimamia afisi za mashinani.

Kulingana naye, viongozi wakuu wa chama hicho waliamua kutoingilia mamlaka ya madiwani.

“Tunataka kusema wazi kwamba chama hiki na kiongozi wa chama hawaingilii na hawataingilia mamlaka ambayo wananchi walikabidhi madiwani kutekeleza majukumu yao yoyote ikiwemo kukagua shughuli za afisi ya gavana,” akasema kwenye taarifa.

Tangu mwaka uliopita, Bw Aladwa amekuwa akiwasilisha barua kwa madiwani wa ODM Nairobi kutoshiriki katika harakati za kumng’oa Bw Sonko mamlakani.

Taarifa aliyotoa jana iliibua mdahalo miongoni mwa wananchi ambao walishangaa kama misimamo ya Bw Sonko katika siku za hivi majuzi ndizo zilimfanya Bw Odinga kumtetea kwa madiwani.

Bw Sonko alianza kwa kusambaza picha zilizomwonyesha akisalimiana na Bw Odinga mapema mwaka huu, kisha akafadhili shughuli za kuhamasisha Mpango wa Maridhiano (BBI) jijini kwa madaha.

Alibandika jumbe za kushabikia BBI kwenye magari yake ya kibinafsi na yale ya kufanya shughuli za utoaji msaada kwa jamii kama vile malori ya kusambaza maji.

Baadhi ya jumbe hizo huandamana na picha za Rais na Bw Odinga.

Kwa msingi huo, watumizi wa mitandao ya kijamii walidai Gavana wa Kiambu, Bw Ferdinand Waititu, angekuwa mjanja na kuunga mkono BBI ili aepuke kutimuliwa.

Kando na hayo, wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema kuna uwezekano Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta hawangependa kuwe na uchaguzi mdogo wa ugavana katika kaunti hiyo.

Jinsi ilivyo kwa sasa ambapo hakuna Naibu Gavana, Bw Sonko akiondolewa mamlakani itabidi Spika wa Bunge la Kaunti, Bi Beatrice Elachi ashike zamu kwa muda kisha uchaguzi mdogo ufanywe kuchagua gavana mpya.

Ikizingatiwa taharuki za kisiasa zilizoshuhudiwa wakati wa uchaguzi mdogo katika eneobunge la Kibra mwaka uliopita, wadadisi wanasema uchaguzi mdogo wa ugavana katika jiji hilo kuu hautatikisa handsheki pekee bali pia Chama cha Jubilee kwa jumla.