Sonko atambua jenerali
Na VALENTINE OBARA
HATIMAYE Gavana Mike Sonko amekunja mkia na kubadili msimamo wake wa awali kuhusu Idara ya Huduma za Nairobi (NMS).
Hii ni baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutisha kumtimua iwapo hatafanya kazi na NMS inayosimamiwa na Meja Jenerali Mohamed Badi.
Julai 2020 Waziri wa Usalama Fred Matiang’i alisema serikali ilikuwa ikifikiria uwezekano wa kuvunja utawala wa Bw Sonko kutokana na migongano kati yake na Bw Badi.
Baadhi ya madiwani waliohudhuria mkutano katika Ikulu wiki mbili zilizopita, ambapo iliamuliwa Spika Beatrice Elachi aondolewe mamlakani, walisema Rais Kenyatta alimuonya Bw Sonko vikali kuwa atafuata Bi Elachi nyumbani asiposhirikiana na Bw Badi.
Bi Elachi alijiuzulu Jumanne katika kile kilichoibuka kuwa ni agizo kutoka kwa Rais Kenyatta katika juhudi za kutuliza mivutano ambayo imekuwepo katika bunge la kaunti na kati yake na Bw Sonko.
Bi Elachi alisema amekabidhi barua ya kujiuzulu kwa Rais, hatua ambayo ni kinyume na kanuni za spika kujiondoa madarakani kwani alifaa kumwandikia karani wa bunge mbali sio kiongozi wa nchi.
Kwa miezi kadhaa tangu alipokabidhi baadhi ya huduma za jiji kwa Serikali Kuu, Bw Sonko amekuwa akishambulia NMS akidai inahujumu mamlaka yake kama gavana.
Hali hii ilimpelekea kushtaki serikali na mahakama ikaamua kulikuwa na ukiukaji wa sheria kuhusu jinsi majukumu ya Kaunti ya Nairobi yalivyokabidhiwa kwa utawala wa Rais Uhuru Kenyatta.
Akihutubu Jumatano katika hafla ya utoaji wa hati miliki za ardhi jijini Nairobi ambayo ilihudhuriwa na Rais Kenyatta, gavana huyo alitangaza uaminifu wake kwa Rais na kushukuru NMS kwa kazi inazofanya jijini.
Alidai kwamba wanaosema yeye hataki NMS wanaeneza uvumi mtupu, kauli ambayo ni uwongo kwani amekuwa akishambulia NMS kila mara.
“Mimi kama gavana wa Nairobi niko nyuma yako Rais. Nashukuru kwa usaidizi ambao umekuwa ukitupatia na kwa miradi ambayo umeleta kupitia kwa NMS. Kuna mambo mengi yamesemwa. Wengine wanaleta propaganda nyingi za uongo eti Sonko hataki NMS,” akasema.
Mnamo Jumanne, ilifichuka kuwa Rais Kenyatta alihusika katika kumshawishi Bi Elachi kujiuzulu.
ONYO KALI
Duru zilizohudhuria mkutano wa Rais na madiwani zilisema alimwonya Bw Sonko kwamba pia yeye atapoteza wadhifa wake kama ataendelea kupinga juhudi za kuboresha huduma kwa wakazi wa jiji hilo kuu kupitia NMS.
“Naomba NMS ishirikiane kwa karibu na utawala wangu kwani tuna ufahamu mwingi kuhusu jiji hili, ili itusaidie kutimiza malengo yetu kwa pamoja,” akasema Bw Sonko.
Katika hotuba yake, Rais Kenyatta alitaka siasa zikomeshwe kuhusu uongozi wa Kaunti ya Nairobi kwa manufaa ya wakazi.
Kulingana naye, wakazi wengi katika jiji hilo wanaishi kwa uchochole ilhali Nairobi husifika kimataifa kuwa na utajiri mwingi.
Miongoni mwa miradi ambayo inalengwa kuboreshwa kupitia kwa NMS ni ukarabati wa barabara, usambazaji wa maji safi bila malipo katika mitaa ya mabanda na ujenzi wa mabomba bora ya kusafirisha maji taka.
“Tulikubaliana kwamba tunataka kusaidiana. Tuweke siasa chini. Kwa wale wanaojaribu kuleta migogoro bure, wajue jukumu letu kama wanasiasa waliochaguliwa na wananchi sio kutusiana bali kusaidia wananchi ili waboreshe hali yao ya maisha,” akasema Rais.
Hafla hiyo iliyofanywa nje ya ukumbi wa KICC ilihuduriwa pia na Bw Badi.
Katika siku za hivi majuzi, Rais Kenyatta amekuwa akiandamana na Bw Badi usiku kukagua baadhi ya miradi ambayo NMS inaendeleza jijini.
Wiki chache zilizopita, Bw Sonko pia alianza kuzindua miradi katika juhudi za kushindana na NMS, ambayo alidai inalenga kujitafutia sifa kwa miradi ambayo serikali yake ilianzisha.