BONFACE OTIENO na FAUSTINE NGILA
TOVUTI kadha za mashirika ya kiserikali Jumatatu zilidukuliwa na kundi la wahuni wa mitandaoni kutoka Indonesia kwa jina Kurd Electronic Team.
Baadhi ya tovuti 18 zilizodukuliwa ni Huduma ya Kitaifa kwa Vijana (NYS), Mfumo wa Usimamizi wa Fedha za Serikali (IFMIS), Tume ya Huduma za Mahakama (JSC), Idara ya Uhamiaji, Tume ya Nyama Nchini, Wizara ya Mafuta, Idara ya Mipango miongoni mwa zingine.
Udukuzi huu ulifanyika asubuhi huku wakora hao wakiweka nembo zao kwenye tovuti walizodukua, ishara kwamba walikuwa wamechukua usukani.
Lakini kufikia Jumatatu saa mbili usiku, Mamlaka ya Habari na Mawasiliano ilikuwa imerudisha tovuti hizo mikoni mwa serikali, baada ya maafisa wa serikali wa teknolojia kudukua tena tovuti hizo kuzirudisha kwa usukukani wa serikali ya Kenya.
Afisa mkuu mtendaji wa shirika hilo Katherine Getao alithibitisha hayo huku akisema katika kisa cha IFMIS, wadukuzi hao hawakuweza kudukua mfumo wenyewe, lakini walifanikiwa kubadilisha tovuti pekee.
Haya yanajiri miaka michache baada ya mdukuzi wa Indonesia kufuta tovuti za serikali zaidi ya 100 nchini humo.