Trump aorodhesha Wakenya 1,282 anaotaka wakanyage nje
SERIKALI ya Rais mpya wa Amerika Donald Trump imetoa orodha ya wahamiaji wanaotakiwa kufurushwa nchini Amerika huku mpango wa kutimua wahamiaji haramu ukianza kushika kasi.
Kulingana na stakabadhi kutoka Idara ya Uhamiaji (ICE) ambazo zimefikia meza ya Taifa Leo, Wakenya 1,282 wameorodheshwa kupakiwa kwenye ndege na kurudishwa Kenya wakati wowote kuanzia sasa.
Stakabadhi hizo zinaonyesha idadi kamili ya wahamiaji kutoka kila nchi ambao wanatakiwa kutimuliwa, huku mataifa ya Amerika Kusini yakiwa na idadi kubwa zaidi ya maelfu ya raia.
Nchi inayoongoza kwa idadi kubwa ya watakaotimuliwa, kulingana na takwimu hizo ni Guatemala 253,413 ikifuatwa na Mexico 252,044 kisha El Salvador 203,822.
Majirani wa Kenya, Tanzania ina wahamiaji 301 watakaotimuliwa, huku Uganda ikiwa na 393.