HabariSiasa

UFISADI: Raila 'amtafuna Ruto mzima mzima'

March 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PETER MBURU

KINARA wa chama cha ODM, Raila Odinga, Jumatano alimshambulia vikali Naibu Rais William Ruto akidai anaingilia uchunguzi wa wizi wa mali ya umma kwa hofu ya kukamatwa kwenye vita hivyo.

Akizungumza siku moja tu baada ya Rais Uhuru Kenyatta kushambulia wanasiasa wanaojitambulisha kuwa wafuasi wa Dkt Ruto, akidai wanatatiza vita dhidi ya ufisadi, Bw Odinga alijitokeza waziwazi na kurusha makombora ya moja kwa moja dhidi ya Naibu Rais.

“Wewe ni nani utwambie pesa zilizoibwa sio Sh21 bilioni bali ni Sh7 bilioni? Ulijuaje? Lazima unafahamu mengi,” akachemka Bw Odinga akihutubia Kongamano la Magavana katika Kaunti ya Kirinyaga.

Akizungumza wiki iliyopita, Dkt Ruto alikanusha habari za Mkurugenzi wa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI), George Kinoti kuwa wanachunguza wizi wa Sh21 bilioni za mradi wa ujenzi wa mabwawa ya Kimwarer na Arror katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet. Alisema ni Sh7 bilioni ambazo zilikuwa zimetumika katika awamu ya kwanza ya mradi huo na hazikuwa zimepotea.

Kauli hiyo ilirudiwa na Seneta Kipchumba Murkomen wa Elgeyo Marakwet aliyedai kuwa DCI inatumiwa kuzima ndoto za Dkt Ruto kushinda urais 2022.

“Wewe ni nani kutwambia kuhusu wizi wa pesa za mabwawa? Wacha mashirika ya uchunguzi yatwambie. Ulijuaje kuhusu kiasi hicho? Wewe haufanyi kazi ya uchunguzi! Tupe muda tupumue,” akasema Bw Odinga.

“Wacha mashirika yenye wajibu wa kupigana na ufisadi yafanye kazi yake. Yametosha! Hakuna aliye juu ya sheria. Kila mmoja abebe msalaba wake bila kuhusisha watu wengine,” akasema.

Akaendelea: “Ikiwa ufisadi umefanyika katika idara fulani, wanaofanya kazi hapo ndio wanaokamatwa. Huwezi kusingizia watu wengine eti ndio kuwe na usawa wa kikabila katika ufisadi.”

Alirejelea matamshi ya Rais kuwa hakuna kiongozi atakayesazwa akibainika kuwa amefanya ufisadi hata awe wa ngazi gani.

Bw Odinga alidokeza visa vya mataifa mengine, ambapo mawaziri wamejiuzulu kwa kuhusishwa na ufisadi na hata wengine kufungwa jela.

“Ikiwa mawaziri kutoka Indonesia na Afrika Kusini wanaweza kujiuzulu, ikiwa watu wa Korea Kusini wanaweza kumfunga Rais aliye madarakani, kwa nini Wakenya wasifanye kitu? Tuelewane kuwa hili litafanyika kwa kila mtu. Kila mtu abebe msalaba wake bila kuwahusisha wengine,” Bw Odinga akasema.

Kwa mara kadhaa sasa, Dkt Ruto amelalamika kuwa kuna watu wanaoingiza siasa katika vita dhidi ya ufisadi.

Viongozi wanaojitambulisha naye pia wamekashifu DCI wakidai inatumiwa kumhangaisha kupitia vita dhidi ya ufisadi.

“Mwanzoni, vita dhidi ya ufisadi vilikuwa vikiendeshwa kwa njia sawa, lakini hilo limebadilika na sasa kuna kitu fiche kwani vinachukua mkondo wa kisiasa. Hatutaketi tena kujionea watu wetu na Naibu Rais wakilengwa. tumeamua!” Mbunge wa Keiyo Kusini, Daniel Rono alisema.

Mbunge wa Chepalungu, Gideon Koskei naye alihusisha matatizo yanayomkumba Dkt Ruto na muafaka baina ya Rais Kenyatta na Bw Odinga.

“Dkt Ruto anapigwa katika mpango wa kutatiza ndoto zake za kutafuta Urais 2022, ili kuwafanya wapinzani wake kumridhi Rais Kenyatta Ikulu,” seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen alisema wiki iliyopita.