HabariSiasa

Uhuru amkausha Ruto kwenye uteuzi

May 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANDISHI WETU

WATETEZI wakuu wa muafaka kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga wamevuna pakubwa kwenye mabadiliko yaliyofanywa katika balozi mbalimbali za Kenya duniani na usimamizi wa mashirika tofauti ya kiserikali.

Arifa kwenye gazeti rasmi la serikali lililochapishwa Ijumaa lilionyesha Rais Kenyatta na mawaziri katika serikali yake, waliteua idadi kubwa ya watetezi wa handsheki katika hali inayosawiri sura ya kitaifa serikalini.

Hii ni tofauti na hali ilivyokuwa kati ya 2013 hadi 2017 ambapo viongozi wa upinzani walikuwa wakilalamikia jinsi nafasi hizo zilikuwa zikipeanwa kwa wandani wa Rais na naibu wake, Dkt William Ruto pekee.

Wakati huu, tathmini ya karibu ya orodha ya walioteuliwa kwenye nyadhifa mbalimbali yaonyesha hakuna wandani wengi wa Bw Ruto walioajiriwa ikilinganishwa na idadi ya wafuasi wa vyama vya ODM, Wiper na KANU kando na wanaounga mkono misimamo ya Rais kuhusu maswala mbalimbali, almaarufu kama ‘Team Kieleweke’.

Miongoni mwa waliojiunga na serikali ni wabunge wa zamani Dennis Waweru (Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Uwekezaji Kenya), Nicholas Gumbo (Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta), na Jamleck Kamau (Mwenyekiti wa Mamlaka ya Ustawi wa Mito Tana na Athi).

Gavana wa zamani wa Kitui, Bw Julius Malombe ambaye ni mwandani wa Kiongozi wa Chama cha Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Shirika la Vyanzo vya Maji Kenya, naye aliyekuwa Seneta wa Tana River, Bw Dan Mwanzo aaichaguliwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Feri Kenya.

Wandani wengine wa Bw Musyoka waliopata ajira serikalini ni aliyekuwa Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Machakos, Bi Susan Musyoka ambaye aliteuliwa kuwa mwanachama katika Kituo cha Rasilimali za Maji yanayochimbwa, na aliyekuwa Mbunge wa Afrika Mashariki, Bw Peter Mathuki.

Bw Musyoka amekuwa akitangaza wazi msimamo wake wa kushirikiana na serikali ya Rais Uhuru Kenyatta tangu Rais alipofanya muafaka na Bw Odinga mnamo Machi 9, 2018 na hata kujitangaza kuwa “mtu wa mkono” wa Rais.

Orodha hiyo na nafasi 82 zitakazojazwa ilionyesha kuna usawa kwa kiwango fulani katika uwakilishi wa maeneo tofauti ya kitaifa kwa kuwa jamii karibu zote za Kenya zimewakilishwa.

Hili linaambatana na msimamo wa Rais na Bw Odinga kutumia ushirikiano wao kuleta umoja wa nchi, ingawa haingeweza kubainika wazi kama walishauriana kabla uteuzi huo kufanywa.

Jana, wakati alipokuwa eneo la Gem, Kaunti ya Siaya, Bw Odinga alirejelea msimamo wake kwamba muafaka wao na Rais utaondoa mgawanyiko wa kijamii ambao umekumba Kenya kwa miaka mingi.